OJADACT YAMPONGEZA WAZIRI MKUU DHIDI YA MAPAMBANO YA DAWA ZA KULEVYA


Na Mwandishi wetu Mwanza

Chama Cha Waandishi wa Habari wa Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) kimepongeza kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuvitaka vyombo vya habari vikemee matumizi ya dawa za kulevya.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya Duniani iliyoadhimishwa Julai 2 mwaka huu na kufanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam, ambapo alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuandika habari za kukemea matumizi ya dawa za kulevya na kutoa habari kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya.


Mwenyekiti wa OJADACT, Edwin Soko amempongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari kweye mapambano ya dawa za kulevya.


"Waziri Mkuu Majaliwa kwanza ametambua kazi zinazofanywa na waandishi wa habari kwenye kupambana na dawa za kulevya na pia amevita vyombo vya habari kuendelea kukemea matumizi ya dawa za kulevya hivyo anatukumbusha wajibu wetu wa kupambana na dawa za kulevya kwa kutumia kalamu zetu", alisema Soko wakati akiongea kwenye kipindi cha jicho letu kinachorushwa na televisheni ya Star TV ya Jijini Mwanza.


Soko aliongeza kuwa, dawa za kulevya hazina majaribio kwani ukionja kuacha ni ngumu na hivyo vyombo vya habari vitoe elimu ya kutosha juu ya athari za madawa ya kulevya ambayo kimsingi yanaathiri mwili, akili na roho.


"Kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa OJADACT tunaitengenezea mkakati wa kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika habari za madawa ya kulevya kwa weledi hivyo tutaandaa muongozo wa kuandika habari hizo ili kuzuia kuchochea na badala yake tuionye jamii kutojiingiza kwenye matumizi ya madawa wa kulevya" alisema Soko.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni tukabiliane na changamoto za dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii.

Mkoani Mwanza, OJADACT ilifanya maadhimisho hayo Juni 30 kwa kuwapa mafunzo waandishi wa habari wa namna bora ya kuandika habari za kulevya.
Mwenyekiti wa OJADACT, Edwin Soko 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments