Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU UTITIRI WA VING’ORA BARABARANI, NAMBA ZA MAGARI


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akipewa kifaa cha kuzimia moto na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma ikiwa ni ziara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) wakati wa ziara ya kikazi, iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi,jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Ayoub Mohamed Mahmoud akipewa kifaa cha kuzimia moto na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga(kulia) baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma ikiwa ni ziara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahomud akipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,John Masunga(kulia) baada ya ziara yake ya kwanza ya kikazi iliyofanyika katika Makao Makuu ya Jeshi hilo,jijini Dodoma.Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Ayoub Mohamed Mahmoud wakikagua mavazi mbalimbali wanayotumia Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kutekeleza majukumu yao.Ziara hiyo imefanyika Makao Makuu ya jeshi hilo,jijini Dodoma.




Na Mwandishi Wetu,DODOMA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema serikali iko mbioni kuweka kampeni ya kudhibiti utitiri wa ving’ora vinavyowekwa katika magari ya watu binafsi ambayo hayatambuliwi na Kanuni za Usalama Barabarani huku pia akigusia namba za magari zinazowekwa katika magari ambayo hayatambuliwi na sheria na kanuni zinazoendesha shughuli mbalimbali za barabarani.

Ametoa rai hiyo wakati wa ziara katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo alifika kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo ambapo aliambatana na Naibu Waziri,Ayoub Mohamed Mahmoud.

‘Gari la Zimamoto linawasha king’ora ili mlipishe liende likatoe huduma ya dharura ya ajali,madereva wengi hawazingatii wala kushtuka na vile ving’ora na kuona kama ni jambo la kawaida,sasa ukikwamisha chombo cha dharura hatua zitachukuliwa dhidi yako na ninawasihi wananchi kuzingatia ving’ora vya gari za wagonjwa,zimamoto,misafara ya viongozi.Na sasa serikali tuko katika hatua za mwisho ili kudhibiti ving’ora ambapo sasa imekua ni vurugu kila mtu anafunga na sasa tunaenda kuviondoa.’ Amesema Waziri Katambi

‘Nchi yetu inaongozwa kwa taratibu na sheria, Jeshi letu la Zimamoto linalaumiwa halifiki kwenye matukio kwa haraka lakini sio kweli,kumekuwepom na watu kutofuata kanuni za ujenzi mtu anajenga kwenye njia,wengine wanakwepa ukaguzi wa vifaa vya zimamoto kwa kukimbia gharama lakini gharama kubwa zaidi ni kupoteza maisha na mali hivyo ndio inatakiwa viwe vipaumbele vya kwanza katika ujenzi wowote ule.Sasa unakuta sehemu kuna janga lakini njia hazipitiki askari wetu watafikaje eneo la tukio?.’ Aliongeza Waziri Katambi

Akizungumza katika ziara hiyo,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Ayoub Mohamed Mahmoud amesema anatambua mchango wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kulinda mali na raia kupitia uokozi huku akiahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano dhamira ikiwa ile ile ya kuwatumikia watanzania.Amewapongeza pia kwa kazi mbalimbali za uokozi ambazo washazifanya katika maeneo mbalimbali nchini.

Nae Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,John Masunga amesema jumla ya matukio ya moto Elfu Tatu na Tisini na Moja yaliripotiwa huku watu Mia Moja Kumi na Nne wakipoteza maisha na majeruhi Mia Mbili Tisini na Tano kwa mwaka ulioisha wa 2025.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com