WANASAYANSI WARIPOTI KUPONA MGONJWA WA NNE WA VVU


Mwanaume ambaye ameishi na virusi vya Ukimwi tangu miaka ya 1980 amepona, madaktari wake wamesema.


Ili kutibu saratani ya damu , mgonjwa alipokea upandikizaji wa uboho kutoka kwa wafadhili ambaye kwa asili alikuwa sugu kwa virusi hivyo.


Mzee ambaye hapendi kutambulika aliacha kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU. Hiki ni kisa cha nne kuripotiwa na wanasayansi.


Mgonjwa alisema " anashukuru sana ” kwamba virusi haviko tena mwilini mwake.


Mwanaume huyo alipokea huduma ya matibabu katika Kituo cha Tiba ya Saratani ya Jiji la Hope huko Duarte, California.


Marafiki zake wengi walikufa kutokana na HIV kabla ya dawa za kurefusha maisha kuwapa wagonjwa muda wa kawaida wa kuishi.

"Sina VVU tena"


VVU huharibu mfumo wa kinga. Hii inaweza kusababisha ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI) kwani mwili una wakati mgumu kupambana na maambukizi.


"Nilipogundulika kuwa na VVU mwaka 1988, kama wengine wengi, nilifikiri kuwa ni hukumu ya kifo.


Sikuwahi kufikiria ningeishi kuona siku ambayo sitakuwa na VVU tena," alisema katika taarifa yake.


Hata hivyo, hakupata tiba hii kwa sababu ya VVU, bali kutibu saratani ya damu ambayo amekuwa akiugua tangu akiwa na umri wa miaka 63.


Timu ya matibabu iliamua kwamba mgonjwa alihitaji upandikizaji wa uboho ili kuchukua nafasi ya chembe zake za damu zenye saratani.


Kwa bahati mbaya, mtoaji alikuwa sugu kwa VVU.


Virusi huingia kwenye chembechembe nyeupe za damu kupitia mlango mdogo sana: protini inayoitwa CCR5.


Hata hivyo, baadhi ya watu, ikiwa ni pamoja na wafadhili, wana mabadiliko katika CCR5 ambayo hufunga mlango na kuzuia kuingia kwa VVU.


Mgonjwa alifuatiliwa kwa ukaribu baada ya kupandikizwa na viwango vya VVU havikuonekana mwilini mwake.


Amekuwa katika uangalizi kwa zaidi ya miezi 17 . "Tunafuraha kukujulisha kwamba VVU yako imepungua na huhitaji tena kutumia tiba ya kurefusha maisha ambayo umekuwa ukitumia kwa zaidi ya miaka 30," alisema Dk. Jana Dickter, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza katika City of Hope.


Hii ilitokea kwa mara ya kwanza mnamo 2011, wakati Timothy Ray Brown, anayejulikana kama "mgonjwa wa Berlin", alikua mtu wa kwanza ulimwenguni kuponywa VVU.


Brown aliishia kufa kwa saratani mnamo Septemba 2020.

Tayari kumekuwa na kesi tatu sawa katika miaka mitatu iliyopita.


Mgonjwa wa City of Hope ndiye mwenye umri mkubwa zaidi kupata matibabu haya na anaishi muda mrefu zaidi na VVU.


Hata hivyo, upandikizaji wa uboho hautaleta mapinduzi katika matibabu ya VVU kwa watu milioni 38 walioambukizwa duniani.


"Ni utaratibu tata wenye madhara makubwa. Hivyo si chaguo sahihi kwa watu wengi wanaoishi na VVU," Dickter alielezea.


Hata hivyo, watafiti wanatafuta njia za kulenga lango la CCR5 , kupitia tiba ya jeni kama tiba inayowezekana.


Kesi hiyo ilifichuliwa katika mkutano wa Ukimwi 2022 huko Montreal, Canada.


"Tiba inasalia kuwa sehemu ya utafiti wa VVU," alisema Profesa Sharon Lewin, rais mteule wa Jumuiya ya Kimataifa ya UKIMWI.


Lewin alikumbuka kuwa kumekuwa na "kesi chache za matibabu hapo awali", ambazo zilitoa "matumaini endelevu kwa watu wanaoishi na VVU na msukumo kwa jamii ya wanasayansi".


Chanzo - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post