SERIKALI YAVUNA BIL 143/- GAWIO AIRTEL

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya Sh Bil 143 ikiwa ni gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Simu ya Airtel, Gabriel Malata (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh (kushoto) jana jijini Dodoma. Wengine Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande (wa tatu kulia) na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza katika hafla ya kupokea gawio lenye thamani ya Shilingi 143 Billioni kutoka kwa Kampuni ya Airtel Tanzania, tukio lililofanyika leo kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma


Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Ltd, Dinesh Balsingh akitoa neno la shukrani kwa Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara katika hafla ya kupokea gawio lenye thamani ya Shilingi 143 Billioni kutoka kwa Kampuni ya Airtel Tanzania Ltd, tukio lililofanyika leo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma

***********************

*Ni matunda ya mazingira bora ya uwekezaji nchini

*Dk Mpango: Taasisi zenye ubia na serikali zijitathmini

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKATI Kampuni ya Mawasiliano ya simu ya Airtel Tanzania Plc ikiikabidhi Serikali Sh bilioni 143 kama gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezitaka taasisi binafsi ambazo Serikali imewekeza hisa hata kama ni asilimia moja kuhakikisha zinajiendesha kwa ufanisi na kulipa gawio stahiki serikalini.

Aidha, amezitaka taasisi zisizotoa gawio kujitathmini kwa kuwa serikali iliwekeza ili faida itumike kwa maendeleo ya wananchi.

"Taasisi ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo bado zinajiendesha kwa faida, lakini hazitoi gawio stahiki zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa gawio serikalini," alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alitoa maagizo hayo wakati akipokea hundi ya Sh bilioni 143 iliyotolewa na Airtel Tanzania Plc kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara. Airtel Tanzania inamiliki asilimia 51 ya hisa zote wakati Serikali ni mmiliki kwa asilimia 49.

Kampuni hiyo kubwa ya pili kwa umiliki wa soko la mawasiliano ya simu nchini, imesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh bilioni 88 ni gawio, Sh bilioni 12 mchango wa uwezeshaji (Support Services Agreement (SSA) na Sh bilioni 43 ni kutokana na mauzo ya minara ya mawasiliano ya Airtel kwenda kwa Minara Tanzania Limited.

Akikabidhi hundi hiyo ya mfano kwa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Airtel Tanzania Plc , Gabriel Malata kiasi cha Sh bilioni 88 ambacho Serikali imelipwa kimeweka rekodi ya kuwa kiasi cha juu kulipwa kama gawio kwa makampuni ambayo Serikali inamiliki hisa.

"Tunapongeza juhudi za Serikali za kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mfumo wa ubia, ambapo leo hii tunashuhudia mafanikio mazuri ya Airtel Tanzania " alisema Malata.

Alisema kwa miaka mitatu sasa, Airtel Tanzania Plc imeweza kulipa Serikali ya Tanzania zaidi ya Sh bilioni 200 zinazotokana na gawio, mchango wa uwezeshaji wa huduma pamoja na malipo mbalimbali. Pia, imeweza kulipa ada na tozo zilizowekwa kwa mujibu wa sheria jumla ya Sh Bilioni 97 kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Akizungumzia maendeleo ya kampuni hiyo, Malata alisema; "Ninayo furaha kukufahamisha kuwa Airtel Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwenye kuunga mkono juhudi mbalimbali za serikali kulingana na hali ya biashara yetu. Kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 Airtel imetoa fursa za ajira zaidi ya 350,000, kati ya hizi zipo ajira za moja kwa moja na zile ambazo sio za moja kwa moja. Nia yetu ni kuendelea kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa manufaa ya Watanzania."

Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio chanya ya kampuni hiyo kufikia kiasi cha kulipa serikalini gawio la Sh bilioni 143.

"Airtel tunaamini kwamba kutokana na Serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji, wawekezaji wazawa na wale wa kutoka nje wataendelea kushirikiana na serikali kama ilivyo kwa Airtel sasa." alisema Malata.

Pia alitoa shukrani kwa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Tume ya Ushindani (FCC), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa mafanikio yote.

Makamu wa Rais, Dk Mpango ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri na endelevu ya kufanya biashara.

Aidha, Dk Mpango alimpongeza Msajili wa Hazina kwa kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yanayowezesha kupatikana kwa fedha na Airtel kuendelea kulipa shilingi bilioni moja kila mwezi.

"Tukio hili la leo linaashiria uwepo wa mazingira mazuri ya kiutendaji na mahusiano thabiti ya kibiashara baina ya wabia. Mapato haya yaliyopatikana yana faida kubwa sana katika kuchangia miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa Watanzania wote. Niwasihi tena tuendeleze jitihada hizi ambazo ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi yetu na manufaa kwa kila mwananchi." alisema Dk Mpango.

Hata hivyo, alitaka kampuni hiyo kujiimarisha na kuendelea kutoa mchango wake kwa manufaa ya taifa na wananchi.

"Hii ni siku nzuri sana kwangu ninaposikia taasisi ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache zinafanya vizuri na kulipa gawio (tena kubwa) kwa serikali kutokana na uwekezaji uliofanyika. Kiasi hiki cha gawio cha Shilingi bilioni 143 kinachotolewa na Airtel kwa Serikali kwa mwaka 2020/21 ni kikubwa na kitasaidia sana katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu."

Naye Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza katika hafla hiyo alisema mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na Bharti Airtel ambayo ilikuwa na mambo makubwa na yenye tija kwa wabia wote na wananchi kwa ujumla wamesimamia vyema na matokeo yanajidhihirisha katika ufanisi wa mapato na michango isiyo ya kodi ambayo wameitoa.

Ofisi ya Msajili wa Hazina ikifuata Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 pamoja na mambo mengine inashauri na kusimamia uwekezaji katika mashirika, taasisi za umma, wakala za serikali na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache sambamba na kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa kutoa gawio na michango mingine serikalini.

Aidha, alisema kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kupata mafanikio katika ukusanyaji wa fedha za serikali.

"Kwa mwaka huu unaoendelea 2021/22, ambapo katika kipindi cha miezi tisa hadi kufikia Machi 2022, Ofisi imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 556 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 106 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 525.49 katika kipindi hicho," alisema.

Airtel Tanzania imekua kwa kasi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kushika nafasi ya pili katika umiliki wa soko, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wateja ambayo imefikia wateja milioni 14.7 na kumiliki soko kwa asilimia 27.2.

Aidha, Airtel Money imefungua zaidi ya maduka 2,000 ya huduma kwa wateja yanayojulikana kama Airtel Money Branches yaliyosambaa mjini na vijijini.

Maduka haya yanatoa huduma na bidhaa ambazo sio tu zinawagusa moja kwa moja wateja, lakini pia yamekuwa suluhisho la huduma za kifedha kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo kwa namna moja hayajafikiwa na huduma za kibenki kwa kujipatia huduma za Airtel Money karibu yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post