COSTECH YAIPATIA TEMDO MILIONI 117 KWA AJILI YA KUTENGENEZA MASHINE YA KUKAMUA PARACHICHI


Mkurugenzi wa TEMDO Mhandisi Fredrick Kahimba akielezea wanahabari baadhi ya mashine zinazotengenezwa na taasisi hiyo ambazo zinalenga kuwainua wananchi.

Na Rose Jackson,Arusha

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imetoa ufadhili wa kiasi cha shilingi milioni 117 kwa ajili ya kutengeneza mtambo wa kisasa wa kukamua parachichi kwa taasisi ya uhandisi na usanifu wa mitambo Tanzania kuanzia kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023.


Utekelezaji wa mradi wa utengenezaji wa mtambo huo umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2021 ambapo unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2023.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko kutoka TEMDO Dkt. Sigsbert Mmasi wakati akizungumza na waandishi wa habari walionufaika na mafunzo ya COSTECH.


Ameeleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakikabiliwa na upotevu wa parachichi na nyingine kuharibika kutokana na ukosefu wa mashine ya kukamulia maparachichi kwa kuwa parachichi nyingi zikiharibika huwa wanazitupa.

Aliongeza kuwa kutokana na ufadhili huo unawezesha TEMDO kuendelea kusimamia mashine hiyo ambayo itawezesha Wakulima kuepukana na upotevu wa maparachichi.


"Mashine hizo tunazitengeneza ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wakubwa na wakati ambapo mkulima mwenyewe anaweza kuchakata parachichi hizo kwa mahitaji yake ya mafuta ya kupikia au kwa ajili ya matumizi ya biashara", alisema Dkt. Mmasi.


Ameeleza kuwa mashine hizo zitatumika Kama shamba darasa ili kuwezesha wakulima kujifunza pamoja na kuwawezesha wajasirimali ambao wanauhitaji waweze kujifunza teknolojia hiyo.


Dkt.  Mmasi alidai kuwa hadi sasa wameshatembelea Viwanda vikubwa vitatu vilivyoko Arumeru lengo likiwa ni kupata taarifa za kubuni teknolojia hiyo ambapo hadi sasa ubunifu wa mashine hizo upo kwenye mchoro na wanatarajia hadi mwezi wa saba watakuwa wamekamilisha utaratibu wa mashine hizo huku mwezi wa kumi na mbili wakitarajia kufanya majaribio ya mashine hizo.

Naye Mratibu wa mafunzo ya habari za Kisayansi na Teknolojia Deusdedith Leonard kutoka COSTECH alisema kuwa kupitia wanahabari wana jukumu la kuhakikisha matokeo ya utafiti yanawafikia wananchi ambao ndio wenye kutumia teknolojia zinazozalishwa na tasisi za utafiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post