WARAIBU DAWA ZA KULEVYA KUPATIWA MAFUNZO YA UKUZAJI UJUZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2022/23 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Machi 30, 2022 katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma iliyokutana kujadili na kupitisha bajeti ya Taasisi hizo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akifafanua jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliyokutana kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 na Makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Machi 30, 2022 katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma .


Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akijibu hoja za wajumbe katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliyokutana kujadili bajeti ya taasisi hiyo Machi 30,2022 Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.


Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dkt. Peter Mfisi akijibu hoja za wajumbe katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliyokutana kujadili bajeti ya taasisi hiyo Machi 30,2022 Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI wakichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichokutana kujadili bajeti za taasisi hizo Machi 30, 2022 Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masula ya UKIMWI na Dawa za Kulevya nchini Mhe. Fatma Taufiq akieleza jambo katika kikao cha Kamati hiyo Machi 30, 2022 katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

(SERA, BUNGE NA URATIBU)

*****************************

Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali imesema inatarajia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu kwa kuwapatia mafunzo ya kukuza ujuzi kupitia vyuo vya ufundi katika fani mbalimbali ili kujiajiri na kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi kuinua kipato chao na kuchangia pato la Taifa.

Hayo yamesemwa Machi 30, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/22 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2022/23 kwa Fungu 91 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Fungu 92 ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma iliyokutana kujadili na kupitisha bajeti ya Taasisi hizo.

Mhe. Pindi alisema Serikali kupitia Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) imepata fedha kiasi cha shilingi billioni 2.4 kwa ajili ya kujenga vituo vitatu (3) vya Serikali vya kutolea huduma za utengamao kwa Waraibu wa dawa za kulevya. Vituo hivi vitajengwa katika Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Tanga.

“Katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imeanzisha Kliniki moja ya Methadone katika Mkoa wa Arusha na ndogo nne katika Mkoa wa Dar es Salaam na kufanya jumla ya Kliniki zilizopo kuwa 15 ambazo zinatoa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini na Ofisi tatu za Mamlaka katika Mikoa ya Dodoma, Mtwara na Mwanza hivyo kupitia programu hii ya kukuza ujuzi wanufaika wa mafunzo hayo watapatiwa zana za kufanyia kazi,”Alisema Mhe. Pindi.

Pia Mhe. Waziri Pindi alifafaua kuwa Serikali inaendelea kufanya Uraghibishi kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo Viongozi wa Kijamii, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Wanafunzi wa shule, Vyuo pamoja na jamii kwa ujumla ili kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“Serikali imezitambua na kuzijengea uwezo Asasi za Kiraia 77 kwenye Mikoa 18 Nchini. Asasi hizi zinafanya kazi ya kuwafuatilia waraibu na kuwaunganisha na vituo vya tiba katika kufikia malengo yaliyokusudiwa ya mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ambazo matumizi yake yamekuewa yakiathiri afya za watumiaji na kuharibu nguvu kazi ya Taifa,”alieleza Mhe. Pindi.

Kwa upande wake Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dkt. Peter Mfisi akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo alieleza kwamba mamlaka itaendelea kufuatilia matumizi ya vilevi watashirikiana na mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha wazalishaji wanazingatia afya za watumiaji huku akihimiza waraibu wa dawa hizo kujitokeza kupata matibabu waweze kurejea katika hali ya kawiada.

“Sisi tunao mpango wa kujenga Kliniki katika Mkoa wa Shinyanga na mara nyingi tunapojenga tunafanya utafiti kwanza wa ukubwa wa tatizo katika eneo husika na hizi Kliniki za Methedone zinatibu tu waraibu wa Heroin kwa kweli tunafanya kila jitihada kuhakikisha mapambano haya yanafanikiwa,”alisisitiza Dkt. Mfisi.

Kuhusu Masuala ya UKIMWI Mhe. Pindi alibainisha kwamba Serikali inatekeleza Kampeni ya FURAHA YANGU inayolenga kuhamasisha upimaji wa VVU kwa wanaume ambapo imesaidia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaopima VVU kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 81 mwaka 2020 wakati lengo ilikiwa ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2023.

“Serikali inashirikiana na Asasi zisizo za kiserikali na wadau mbalimbali katika upimaji na tohara kwa wanaume kupitia Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2018/19-2022/23,”alifafanua Mhe. Pindi.

Vile vile Mhe. Pindi alisisitiza kwamba elimu ya lishe imetolewa kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika Konga 180 kupitia Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kwa kuzingatia makundi 5 ya vyakula ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kulima mazao yanayoweza kuwapatia chakula bora.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mhe. Fatma Taufiq alieleza kwamba baada ya wajumbe kujadili bajeti ya taasisi hizo imepitisha kwa kauli moja Makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa fungu 91 ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na fungu 92 ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kiasi cha shilingi Bilioni 26.9.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments