RUWASA SERENGETI YAFANIKIWA KUPATA CHANZO CHA MAJI KILICHOTAFUTWA KWA MIAKA 9



Chanzo cha maji kikichimbwa

Diwani kata ya Kebanchabancha Philemon Matiko


Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) wilaya ya Serengeti,Mhandisi Deus Mchele
***
Na Dinna Maningo, Serengeti

CHANZO cha Maji kilichotafutwa tangu mwaka 2013 katika kijiji cha Kebanchabancha kata ya Kebanchabancha wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kimepatikana na kwamba wanachi watanufaika na huduma ya maji safi na salama waliyoikosa baada ya chanzo cha maji kilichokuwepo kufunikwa na Maporomoko.

Waandishi wa Habari waliofika katika wilaya hiyo, walikitembelea chanzo hicho cha maji nakushuhudia mafundi wakiwa kazini wakichimba kisima kwa kutumia mitambo ya kisasa na maji kuonekana.

Paul Zakaria mkazi wa kijiji cha Kebanchabancha alisema kuwa ukosefu wa chanzo cha maji cha huhakika kulisababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma ya maji kwakuwa chanzo kilichopo wakati wa kiangazi hukauka.

"Wananchi tunateseka na maji wakati wa kiangazi kikipiga sana kisima kinakata maji inabidi tutafute maji kwenye visima vya mbali,kupatikana kwa chanzo hiki cha maji kutaondoa adha kwa wananchi" alisema Paulo.

Diwani wa kata ya Kebanchabancha Phillemon Matiko anaeongoza kata hiyo kwa miaka 22 hadi sasa,alisema kuwa kisima kilichotumika kama chanzo cha maji hakitoshelezi mahitaji kwakuwa wakati wa kiangazi hukauka.

"Hiki kijiji kimezungukwa na milima hivyo maji hayakuweza kupanda milimani ili kuwafikia wananchi,ikabidi wataalamu wa maji watafute chanzo kingine cha maji kimetafutwa sana bila mafanikio lakini mwenyezi Mungu kajalia kupitia wataalamu wetu wa RUWASA chanzo kimepatikana na nyie waandishi wa habari mmeshuhudia maji yakitoka kwa wingi.

" Tunatafuta maji kwenye visima vya asili na visima vilivyochimbwa na watu wa AMREF mwaka 2008,tenki la maji lipo km 5 kutoka kwenye chanzo cha maji ambacho kimefunikwa na maporomoko nakusababisha tenki likose maji"alisema Diwani.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) wilaya ya Serengeti,Mhandisi Deus Mchele alisema kuwa tenki la maji limegharimu Milioni 500 tangu 2013 nakwamba kwa mwaka wa fedha 2021-2022 serikali imetoa fedha Milioni 200 kwa ajili ya kuchimba chanzo kipya cha maji na kutengeneza mfumo mzima wa maji kutoka kwenye chanzo cha maji kwenda kwenye tenki,kununua mashine na kuweka mabomba.

"Tangu mwaka 2013 tunahangaika kupata chanzo cha maji,chanzo cha maji kilichokuwepo kiliharibika baada ya kutokea maporomoko lakini sasa kimepatikana, kampuni ya Target Boreholes imechimba na chanzo hiki kina urefu wa mita 150 kutoka chini,maji yameonekana na kina uwezo wa kutoa Maji lita 8000-10,000 hadi kufikia juni,2022 mradi utakuwa umekamilika.

Mchele alisema kuwa mradi huo ulishajengwa imebaki tu hatua ya ukamilishaji wa chanzo cha maji ili kusambaza maji kwenye vituo 6 katika kijiji cha Kebaanchabancha chenye wakazi 2912 na kijiji cha Sogoti chenye wakazi 1889.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments