AGONGELEWA KWENYE MTI KWA MISUMARI KAMA YESU AKISULUBIWA MADAI YA KUIBA REDIO Polisi wameanzisha msako mkali ili kumkamata mshukiwa aliyempigilia misumari katika mikono ya mwanaume mmoja mwa madai ya kuiba redio katika Kaunti ya Vihiga nchini Kenya.

Collins Sambaya mwenye umri wa miaka 19 alipatikana mikono yake miwili ikiwa imepigiliwa kwenye mti kwa misumari ya kuezeka paa mfano wa Yesu akisulubiwa. 

 Sambaya alinusuriwa kwa mashine ya kukata miti huku mshukiwa akikimbilia mafichoni alipowaona polisi wakifika eneo la tukio.

 Collins Sambaya aliyedaiwa kuiba redio alipatikana mikono yake yote ikiwa na misumari ya kuezeka paa katika kijiji cha Chemasili, Sabatia, Kaunti ya Vihiga

“Katika kisa ambacho kiliduwaza kijiji cha Izava eneo la Sabatia, Collins Sambaya mwenye umri wa miaka 19 alipatikana mikono yake ikiwa imepigiliwa kwa mti kutumia misumari ya kuezeka,” Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema.


Wakaazi walimuarifu Chifu wa kata ya Izava Kaskaini Evans Endesha ambaye aliwaapa taarifa maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kilingili.

 Ripoti zinaarifu kuwa mshukiwa alikimbilia mafichoni baada ya kuwaona maafisa wa polisi wakiwasili eneo la tukio.

 “Msako umeanzisha kuwakamata washukiwa waliotekeleza unyama huo. Vikosi vya usalama eneo hilo inatumia kila mbinu kuhakikisha kuwa washukiwa wananaswa,” taarifa hiyo ya DCI iliongeza. 

Kwa mujibu wa picha za video, wakaazi chini ya uangalizi wa maafisa wa polisi, walijaribu kumwondoa Sambaya kutoka kwa mti huo kwa kutumia mashine ya kukata miti.

Juhudi zao zilifua dafu, Sambaya akiokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbale kwa matibabu ambako amelazwa akiwa kwa hali nzuri. 

“Wanakijiji walipigwa na butwaa kwa kile kilichokuwa kimempata mwenzao walitazama kwa mbali maafisa wa polisi wakimwokoa na kumkimbiza hospitalini,” DCI iliongeza.

Chanzo - Tuko Swahili 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post