ALIYEACHANA NA MME SUMBAWANGA NA KUOLEWA NA MWINGINE AJIFUNGUA MKONO WA MAMBA...AKOJOA MJUSI


Mfano wa mkono wa mamba na mjusi

Na Ibrahim Yasin - Kyela
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Maria Mwakila (26), mkazi wa Kitongoji cha Mbyaso, Kijiji cha Mpunguti, Kata ya Ikama wilayani Kyela mkoani Mbeya, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kutokwa na mjusi sehemu za siri alipokwenda kujisadia haja ndogo.

Wiki tatu zilizopita, binti huyo aliripotiwa kujifungua mkono wa mamba na kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo. Ilidaiwa kuwa kijana huyo alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na alitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela baada ya kukumbana na mkasa huo.

Siku 18 baada ya kupata matibabu hayo, jana majira ya saa mbili asubuhi, alipokwenda kujisaidia haja ndogo, alidai ulitoka mjusi ukiwa na kucha mkiani.

Akizungumza jana na Nipashe Jumapili baada ya kumaliza kikao cha machifu, mume wake, Lugano Sindalama, alisema walioana Oktoba mwaka jana baada ya kuwa ameachana na mwanamume aliyekuwa naye wilayani Sumbawanga.

Mume wake huyo alidai kuwa baada ya kupata ujauzito, mke wake alikumbana na matatizo mengi ikiwamo kuugua mara kwa mara.

Alisema kuwa ilipotimu miezi mitatu ya ujauzito huo, alianza kujisikia dalili za uchungu na walipomwahisha hospitalini alipona na kurejea nyumbani lakini siku hiyo hiyo aliyotoka hospitalini, akiwa sebuleni, alijisikia kama ameshikwa na haja ndogo, alipofika eneo la kujisitiri, alijikuta akitokwa na mkono wa mamba huku damu nyingi ikimtoka.

Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo ilibidi akimbizwe hospitalini na kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kusafishwa tumbo ambapo waliondoa uchafu uliokuwamo na baada ya wiki tatu akiwa katika hali safi na salama akajikuta anajisaidia mjusi ulio na mkia wenye kucha.

Alisema baada ya hapo wazee wa kimila waliitisha kikao cha machifu na familia zao kujadili sintofahamu hiyo na namna ya kuidhibiti.

Atupakisye Mwamakula, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, alisema ni tukio la kwanza kutokea katika eneo lao na pia waliposikia mwanamke amejifungua mkono wa mamba waliona ni jambo la kawaida kwa kuwa maeneo mengi huwa yanatokea.

Alisema kuwa tukio la pili walipolisikia amejisaidia mjusi, walishikwa na butwaa ndipo walipoitisha kikao ili wajue tatizo na kulitafutia ufumbuzi.

Akizungumzia hali hiyo, Maria alisema anamwachia Mungu, akiamini ipo siku atajifungua mtoto wa kawaida asiyekuwa na dosari.

Chifu Mkuu wa Kijiji hicho, Magojanya Mwaluswa, alisema wamekemea kitendo hicho na kushauri familia zinazovutana na kuwa kile wanachoamini ni kiini cha tatizo, zimalizane kwa kuwa kijiji hicho na vitongoji vyake havina historia ya matukio hayo.

CHANZO - NIPASHE

    Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

    Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

    0/Post a Comment/Comments