WATU 13 WAUAWA KWA BOMU LILILOTEGWA ARDHINI WAKIWA KWENYE DALADALATAKRIBANI watu 13 wamefariki dunia kufuatia mlipuko uliotokea leo, Januari 31, 2022 asubuhi katika eneo la Mandera, Kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Somalia baada ya gari la abiria (daladala) kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini ikiwa ni siku mbili tu baada Ufaransa kutoa tahadhari ya Shambulio.

Watu wengine kadhaa ambao idadi yao haijafahamika wamejeruhiwa. Gari hilo lilikuwa likisafiri kuelekea Mandera, Mji ulio katika eneo la mpakani, ambao umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mashambulizi ya wanamgambo.

Picha kutoka kwa wanahabari wa eneo hilo zinazoshirikishwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha mabaki ya gari la umma, linalojulikana kama matatu, ambalo lilipuliwa baada ya kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa barabarani.

Hakuna aliyedai kuhusika, lakini waasi wa Al Shabaab wamekuwa wakiwalenga polisi na raia ndani na karibu na Mandera na vifo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, na kuifanya Mandera kuwa moja ya maeneo hatari zaidi ya Kenya kuishi.

Shambulio hilo limetokea wiki moja tu baada ya balozi kadhaa za kigeni nchini Kenya, zikiwemo Marekani na Ufaransa, kuwaonya raia wake kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments