RPC SHINYANGA APIGA MARUFUKU DISKO TOTO, KUCHOMA MATAIRI ..."WALEVI KULA SIKUKUU YA KRISMASI NA MWAKA MPYA MAHABUSU"


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Desemba 23,2021. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Desemba 23,2021

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Katika kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya 2022 Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga limepiga marufuku Disko Toto pamoja na ulipuaji wa baruti, fataki na uchomaji matairi huku likiwataka wafanyabiashara wa maduka makubwa yakiwemo ya Fedha yafungwe mapema sambamba na kuweka walinzi ili kuepuka mianya ya wahalifu kutumia Sikukuu kufanya uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 23,2021 wakati akitoa salamu za Krismasi na Mwaka Mpya 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati za sherehe hizo.

Amesema licha ya kwamba jeshi la polisi limejipanga ipasavyo lakini bi vyema wananchi wakaendelea kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa za viashiria vya matukio ya uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari kuzuia vitendo vya uhalifu katika jamii.

“Jeshi la polisi limeimarisha doria za magari,pikipiki na doria za miguu, tutalinda sehemu zote za ibada na mikesha na maeneo yote yenye mikusanyiko halali ikiwemo ya burudani na misako mikali itafanyika sehemu mbalimbali zenye maficho ya wahalifu”,amesema Kamanda Kyando.

“Disco toto kwenye kumbi zimepigwa marufuku, haziruhusiwi kabisa hivyo yeyote mwenye nia hiyo afute wazo hilo. Ulipuaji wa baruti, fataki na uchomaji matairi vitendo hivyo vyote vimepigwa marufuku”,amesema.

Kamanda Kyando pia amewatahadharisha watumiaji wa pombe kujiepusha na ulevi wa kupindukia kwani unaweza kuwapelekea kusherehekea sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya wakiwa mahabusu au magereza kabisa.

“Watumiaji wote wa vyombo vya moto wanatahadharishwa kufuata sheria za usalama barabarani hasa waendesha pikipiki,bajaji na magari. Pia wajiepushe na matumizi ya vilevi kwani upimaji wa walevi utafanyika kwa nguvu sana”,ameeleza.

Aidha amewataka wenye nyumba kufunga nyumba zao kwa uimara au kuacha mtu wa kulinda nyumba hiyo badala ya kuacha watoto kuwa walinzi

“Walinzi wa makampuni binafsi na watu binafsi kuwa makini sana kwa siku hizi za sikukuu wajiepushe kuingia malindoni wakiwa wamelewa,kuongea na watu wasio wajua kwenye maeneo yao ya ulinzi na kula au kupewa chochote na mtu ambaye hawajakubaliana kufanya hicho kitu”,amefafanua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments