BADEA KUIPAISHA TANZANIA KIMAENDELEO KWA SH. TRILIONI 7 MIAKA MITANO IJAYO


Na Benny Mwaipaja, Cairo
BENKI ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) imeahidi kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu pamoja na misaada inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu sawa na takribani shilingi za Tanzania trilioni 7 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ahadi hiyo imetolewa Jijini Cairo Nchini Misri na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dkt. Sidi Ould Tah alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

“Tumekuwa na majadiliano ya kina na yenye tija na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania pamoja na ujumbe wake ambapo tumejadili mambo mengi ya msingi kwa ajili ya uhusiano wetu kama Benki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tuko tayari kutoa fedha hizo” alisema Dkt. Tah.

Alifafanua kuwa fedha hizo zitatolewa katika kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo katika maeneo matano ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu, kilimo, kuimarisha sekta binafsi pamoja na kuwajengea uwezo wataalam.

“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla kwa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa n chi yake na sisi tunaahidi kwamba tutashirikiana naye katika mipango yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa kuamua kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho kitasaidia kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka kupitia miradi ya kimkakati waliyokubaliana kupatia fedha hizo.

Alisema kuwa BADEA ni wadau wakubwa wa maendeleo nchini ambapo mpaka sasa wametoa mikopo na misaada inayofikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.24 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ukiwemo mradi mkubwa wa maji uanaoanzia Mwanga kwenda Same mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Mwigulu alisema kuwa mikopo na misaada ya dola za marekani bilioni 3 zitakazotolewa na Benki hiyo katika kipindi cha miaka 5 ijayo zitatumika kuboresha Nishati, ujenzi wa miradi zaidi ya 14 ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na ujenzi wa barabara zitakazofungua fursa za kiuchumi kwenye maeneo yanayozalisha bidhaa zikiwemo za kilimo.

“Fedha hizi ambazo BADEA watatupatia zitatumika pia kuendeleza sekta binafsi ambapo benki zitapatiwa sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu kwenye sekta za uzalishaji na kukuza ajira kwa vijana na wanawake kupitia shughuli mbalimali ikiwemo biashara na shughuli nyingine za ujasiliamali” alisema Dkt. Nchemba.

Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Jamal Kassim Ali alisema kuwa Zanzibar itanufaika na sehemu ya fedha hizo za mikopo nafuu na misaada ambapo kiasi cha dola za Marekani milioni 450 kitatumika kutekeleza miradi kadhaa ya kimkakati.

Aliitaja baadhi ya miradi ambayo fedha hizo zitaelekezwa kuwa ni Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Kisiwani Pemba ukihusisha njia ya kurukia ndege na jengo la abiria, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, ujenzi wa vyuo vya ufundi vitano vya VETA pamoja na maghala ya kuhifadhia mafuta.

Dkt. Ali alisema kuwa hatua hiyo itachangia kusisimua zaidi uchumi wa nchi na pia kukuza ajira ambazo ni changamoto kubwa hivi sasa na kuishukuru Benki hiyo ya Maendeleo ya nchi za Kiarabu BADEA kwa uamuzi huo wa kutoa fedha kuchangia maendeleo ya nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments