JAMAA AUA MKE NA WATOTO WANNE KISHA KUJISALIMISHA POLISI
Mwanaume mmoja, Paul Murage mkazi wa Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya, anashikiliwa na jeshi la polisi nchini humo akituhumiwa kumuua mkewe, Millicent Muthoni na wanae wanne.

Mtuhumiwa huyo amepandishwa katika Mahakama Kuu ya Kerugoya ambapo jaji anayesikiliza kesi hiyo, Justice Mwongo amesema atalazimika kuendelea kuhifadhiwa katika Gereza la Kerugoya kwa siku arobaini zaidi mpaka januari 24, 2022 kufuatia maombi ya wakili wa upande wa mashtaka, Vincent Mamba aliyeomba muda zadi ili kukamilisha upelelezi.

Murage anatuhumiwa kumuua mkewe na wanae wanne Jumapili ya Desemba 12, 2021 kabla ya kujaribu kujiua huku sababu za mauaji hayo zikiwa bado hazifahamiki.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alijisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi Kianyaga ambapo polisi walipoenda nyumbani kwake, waliikuta miili ya mkewe na wanaye, Nelly Wawira mwenye umri wa miaka 13, Sheromit Wambui Muthoni mwenye umri wa miaka 5, Gifton Bundi Muthoni mwenye umri wa miaka 7 na Clifton Njuki Murage mwenye umri wa mwaka mmoja.


Taarifa za polisi zinaeleza kuwa miili hiyo ilikutwa kwenye vitanda vyao, ikiwa na majeraha mengi ya kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali kwenye vichwa vyao.


Kwa mujibu wa kiongozi wa mahali tukio hilo lilipotokea, Murimi Ndambiri, mtuhumiwa huyo alikuwa akijihusisha na biashara na matumizi ya bangi na mara kwa mara alikuwa akimfanyia mkewe na wanaye vitendo vya unyanyasaji.


Kwa mujibu wa kaka wa mtuhumiwa huyo, Patrick Njiru, mke wa mdogo wake alifika nyumbani hapo Jumamosi jioni akiwa na wanaye na kuwaeleza ndugu hao kwamba mumewe alikuwa ametishia kumuua yeye pamoja na watoto na kwamba alikuwa akihofia usalama wao.


Akawaeleza kwamba anataka kumtoroka mumewe huyo ili kuokoa maisha yao na alipoondoka na kurejea nyumbani kwake kwa ajili ya taratibu za kutoroka na wanaye, ndipo tukio hilo lilipotokea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments