WANAFUNZI WALIOPATA UJAUZITO SASA RUKSA KUENDELEA NA MASOMO TANZANIA


Na Dotto Kwilasa, -Malunde 1 blog DODOMA.

SERIKALI ya Tanzania imewaondolea vikwazo  wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari  waliokatisha  masomo yao  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi mara baada ya kujifungua mwaka unaofuata.


Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatano  Novemba 24,2021,na Waziri wa Wizara hiyo,Prof.Joyce Ndalichako wakati akitaja mafanikio ambayo imeyapata Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara na kusema kuwa hatua hiyo  itatoa fursa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopewa ujauzito kurejea shuleni kupata haki yao.


Prof. Ndalichako amesema Wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa Serikali mara baada ya kujifungua.


“Serikali imeamua wanafunzi  waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni itajumlisha wasichana wanaopata ujauzito wakiwa katika shule za msingi na sekondari ,Wanafunzi hao wataruhusiwa kuendelea na masomo yao katika mfumo rasmi wa Seriakali mara baada ya kujifungua,”amesema.


Pia amesema wanafunzi wanaofeli,kufanya udanganyifu au utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari.


“Utaratibu ulivyo sasa mwanafunzi anapofutiwa mtihani wake wa darasa la saba au ambao  watafaulu kufeli mtihani wa darasa la saba au anapokuwa amepata tatizo lolote wakati wa mtihani wa darasa la saba atakuwa hana fursa nyingine,sasa tumeamua wanafunzi wanaofeli,kufanya udanganyifu au utovu wa nidhamu watapewa fursa ya kurudia mitihani na watapewa fursa ya kujiunga na shule za sekondari,”amesema.


Aidha,Prof. Ndalichako amezitaka shule ambazo zinawachangisha wanafunzi fedha za michango kuachana na utaratibu huo kwa sababu msimamo wa Serikali ni kutoa elimu bila malipo.


Aidha,Waziri Ndalichako amesema Mwelekeo wa Sekta ya Elimu baada ya Miaka 60 ya Uhuru wa nchi  ni kuendelea kutoa elimu bora itakayoipatia jamii maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.


Amesema Serikali itahakikisha kwamba inaboresha mitaala ya elimu katika ngazi zote na kuweka msisitizo zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sayansi, Ujasiriamali, Stadi za kazi na masuala mtambuka.


Waziri Ndalichako amesema fani za kimkakati kama vile uhandisi, kilimo, udaktari zitaendelea kupewa kipaumbele.


Amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule ili kuendelea kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume.


“Kazi hii inafanyika kwa kasi zaidi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo sambamba na ujenzi wa madarasa 15,000 unaoendelea nchini Serikali inatarajia kujenga shule 1,000 za sekondari za kutwa na  shule za sekondari 26 za wasichana katika kipindi cha miaka mitano ijayo,”amesema.


Waziri huyo amesema utekelezaji umeanza kwa shule 274 za kutwa na shule 10 za Wasichana ambapo serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 1,405 mnamo tarehe Novemba, 2021.


Licha ya hayo amezungumzia elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuwa itaendelea kuimarishwa ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 29 na Mikoa.


Amesema  lengo ni kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.


“Kwa msingi huo,mafunzo kwa vitendo yatapewa uzito stahiki sambamba na kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira;,”amesema


Prof. Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuimarisha elimu maalum kwa kuhakikisha miundombinu inayojengwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.


Aidha, Serikali itaendelea kununua vifaa visaidizi ili kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza kwa ufanisi zaidi.


Amesema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa fursa za elimu ambapo wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali watapewa fursa ya kurejea shuleni.

 Fursa hizo zitajumuisha wasichana ambao wanapata ujauzito wakiwa katika shule za msingi au sekondari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments