JAMAA AFARIKI BAADA YA KUNYWA POMBE BAA



Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo mwanaume mmoja alifariki dunia nje ya baa muda mfupi tu baada ya kunywa pombe.

Kisa hicho kimetokea katika Kaunti ya Garissa nchini Kenya na kuripotiwa na meneja wa baa hiyo ya 3D Fredrick Thiong’o Mahira ripoti ya K24 ilisema. 

Katika taarifa yake kwa polisi, Thiong’o alisema kuwa alifahamishwa na watu waliokuwa wakijivinjari kuwa kulikuwepo na mtu ambaye alikuwa amelala nje ya klabu hiyo. 

“Akiwa klabuni alifahamishwa kuwa kuna mtu aliyepoteza fahamu alikuwa amelala nje ya klabu. Alipoenda kumchunguza mtu huyo, mwanzoni alidhani alikuwa amelewa tu na ndiyo maana alikuwa amelala akiwa hajitambui,” taarifa hiyo ilisema.

 "Majira ya saa nne usiku meneja huyo alirudi na kuangalia tena lakini akapata mtu huyo bado amelala mahali alipokuwa na hajasonga hata hatua moja," ripoti hiyo iliongeza.

Mara tu meneja wa klabu alipogundua kuwa mtu huyo hasongi wala kujibu lolote, aliwaita askari kutoka Kituo cha Polisi cha Garissa ili kuwaarifu kuhusu kisa hicho. 

Maafisa wa polisi waliofika eneo la tukio walimkagua na kubaini kwamba alikuwa fundi wa Maabara katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Iftin.

 Baadaye afisa huyo alikagua eneo la tukio kabla ya mwili huo kuhamishwa hadi katika makafani ya Hospitali ya Mwingi Level Five ikisubiri uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake. 

Tukio hilo linajiri wakati visa vya watu kuaga dunia baada ya kunywa pombe au kupoteza fahamu kwa saa nyingi vikiwa vimeongezeka. 

Wiki mbili zilizopita, mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Ahmed Karim Abdi alianguka na kufariki dunia katika klabu kimoja maarufu mjini Kitale baada ya kunywa pombe.

 Uchunguzi wa tukio hilo ulibaini kuwa marehemu alikuwa na ugonjwa wa pumu na alikuwa amekunywa pombe kupita kiasi.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments