WATU 6 WA FAMILIA MOJA WAPOFUKA GHAFLA KATIKA MAZINGIRA TATANISHI


Wakazi wa kijiji cha Thim Jope, Uriri, kaunti ya Migori nchini Kenya wamepigwa na bumbuwazi baada ya watu wa familia moja kupofuka katika hali tatanishi.

Katika kisa kisichokuwa cha kawaida, Hellen Achieng' na wanawe wanne wenye umri wa kati ya miaka saba na 24 walipofuka ghafla kabla ya kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori kwa matibabu.

George Omondi aliambia Nation kuwa mpwa wake mwenye umri wa miaka 12, ambaye alikuwa anaishi na familia hiyo, alianza kutetemeka baada ya kupoteza uwezo wa kuona na kisha baadaye alizirai na kufariki dunia.

Omondi aliongezea kuwa mnamo Ijumaa, Novemba 26,2021 mke wake na wanae watano walikwenda kulala wakiwa buheri wa siha.

 Hata hivyo, asubuhi ya siku iliyofuata, walianza kulalamika kuwa wamepoteza uwezo wa kuona.

Akithibitisha kisa hicho, Chifu Msaidizi wa kata ya Thim Jope, Kerry Otieno alisema mwili wa mvulana huyo ulipelekwa katika makafani ya Hospitali ya Misheni ya Ombo.

Aliongeza kuwa bado hawajapata chanzo cha masaibu yanayokumba familia yake. Kabla ya kukimbizwa hospitalini, familia hiyo ilikuwa imewaalika viongozi wa kidini.

 Madaktari nao hospitalini wanajaribu kutafuta chanzo cha upofu wa familia hiyo.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments