TANZANIA, RWANDA NA BURUNDI WARIDHISHWA NA KASI YA UJEZI WA MRADI WA RUSUMO


Na Zuena Msuya, Kagera
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa Mawaziri wa Nishati wa Rwanda, Burundi na wenyeji Tanzania wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa RUSUMO licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

Wakili Byabato alisema hayo wakati akimuwakilisha Waziri wa Nishati, January Makamba, mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 13 wa Mawaziri hao wenye lengo la kujadili maendeleo ya ujenzi wa mradi wa RUSUMO uliofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera, Octoba 9, 2021.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Miundombinu Rwanda, Balozi Claver Gatete ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato na Waziri wa Mafuta, Nishati na Madini wa Burundi, Mhandisi Ibrahim Uwizeye pamoja na Wajumbe wa Bodi wa Mradi huo.

Mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 80, ambazo zitagawanywa katika nchi hizo tatu wanufaika ambapo kila moja itapata Megawati 26.6 kwa ajili ya matumizi ya nchi yake.

Alisema kuwa mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 82 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo tayari mkandarasi amekwisha lipwa zaidi ya asilimia 100% ya kazi aliyokwisha fanya huku kazi ya ujenzi ikiendelea vizuri.

“Tumejadili kwa pamoja maendeleo ya ujenzi wa mradi huu wa Rusumo, tumeridhishwa na kasi ya ujenzi unavyoendelea, pia fedha za kuhakikisha mradi huu unakamilika kama ulivyopangwa zipo tayari, makubaliano ya awali ilikuwa mkandarasi alipwe Dolla 75 kwa kazi aliyofanya lakini aliongezewa kazi pamoja na mbadiliko ya bei ya vifaa hivyo amelipwa Dolla 89, sawa na 114% na hivyo mkandarasi ataendelea kulipwa malipo yake kulingana na kazi anazofanya kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo”, alisema Wakili Byabato.

Hata hivyo alisema kuwa changamoto ya kuwepo kwa Virusi vya Corona Duniani kumesababisha baadhi ya vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa mradi huo kuchelewa kufika kwa wakati kwa kuwa vingi vinatoka nje nchi.

Aliweka wazi kuwa mradi huo umegawinyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni Eneo la Bwawa, Njia ya kuchepusha maji kwenda katika mitambo kuzalisha umeme ambayo ipo upende wa Tanzania, na nyingine ni eneo Kituo cha Kupokea na  Kusambaza umeme ambacho kiko upande wa Rwanda.

Alifafanua mradi huo awali ulikuwa ni kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza umeme tu kwa nchi husika, lakini kwa sasa kituo hicho kimeongezewa uwezo wa kupokea umeme kutoka sehemu zingine na kuusambaza,ambapo kitakuwa na uwezo wa kupokea hata ule umeme utakaozalishwa katika Mradi wa Julius Nyerere na kusambaza katika nchi za Rwanda, Burundi nakadhalika.

Utekelezaji wa hatua ya ujenzi wa kituo hicho cha kupokea na kusambaza umeme ambacho kiko upande wa Rwanda umekamilika kwa asilimia kubwa.

Sambasamba na hilo alisema kuwa kwa nchi zote zitakaotumia umeme utakaozalishwa katika mradi wa RUSUMO ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi zinaendelea na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka katika mradi huo hadi katika maeneo husika.

Mradi wa RUSUMO unatekelezwa kwa gharama za Dolla za Kimarekani Milioni 340 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kwa ushirikiano wa nchi tatu wanufaika ambapo kila moja italipa Dolla Milioni 113.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments