MWANAMKE AKAMATWA NA HEROINE GRAMU 728.5 AKISAFIRISHA KAMA VITABU SINGIDA


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella A. Mutabihirwa akionyesha vitabu vilivyo tumika kufungashia madawa ya kulevya aina ya heroine
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella A. Mutabihirwa akionesha Vitabu vilivyo kuwa vimewekewa madawa ya kulevya aina ya heroine tayari kwa kusafirishwa kama vitabu.

Na Edina Malekela,Singida.
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia msichana aitwaye Dorin Finan mwenye umri wa miaka 25 kwa tuhuma ya kupatikana na madawa ya kulevya aina ya heroine yenye uzito wa gramu 728.5 aliyoyafunga kwenye vitabu ili asafirishe kama mzigo.

Tukio hilo limetokea jana Oktoba 8,2021 Mtaa wa Stendi ya zamani mjini Singida ambapo mtuhumiwa huyo mkazi wa Tabata Bima Jijini Dar es salaam alikamatwa akiwa na madawa ya kulevya yanayodhaniwa kuwa ni aina ya heroine akijiandaa kusafirisha kwenda China.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella Mutabihirwa alisema ukamataji wa madawa hayo umetokana na taarifa walizozipata kutoka kwa wakala wa Kampuni ya usafirishaji mizigo ijulikanayo kwa jina la DHL tawi la Singida,ambapo watuhumiwa wanaosadikiwa kuwa wawili walifika ofisini hapo kwa lengo la kusafirisha madawa hayo yaliyokuwa yamefungwa kwenye vitabu na kuwekwa kwenye bahasha kama mzigo.

Alisema mfanyakazi mmoja wa kampuni hiyo baada ya kuupokea mzigo huo aliutilia mashaka ndipo alipoamua kutoa taarifa Polisi ambapo baada ya taarifa hiyo Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja huku mtuhumiwa mwingine kufanikiwa kutoroka.

"Mbinu waliyoitumia ni kubandua kurasa za vitabu na kuweka madawa hayo kisha kubandika tena na kuonekana kama kitabu kumbe ndani yake kuna madawa.. juhudi za kumsaka mtuhumiwa mwingine zinaendelea na huyu mwingine tunaendelea kumshikilia kwa mahojiano zaidi", alisema Kamanda.


Jeshi la Polisi limetoa wito kwa taasisi ama makampuni yanayojihusisha na usafirishaji wa mizigo ama abiria kuendelea kutoa ushirikiano katika kuibua uhalifu ili kuweza kukabiliana nao kabla haujaleta madhara kwa jamii,huku likiwataka wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwani vitendo hivyo vinasababisha uvunjifu wa amani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments