MPINA AFICHUA KILICHOIBEBA MEATU NA SIMIYU KUONGOZA UKUSANYAJI WA MAPATO AMTAJA RC KAFULILA

 
 Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na Halmashauri ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kuongoza katika ukusanyaji mapato katika kipindi cha robo mwaka.

 

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, Mhe. Luhaga Joelson Mpina amesema usimamizi makini, ufuatiliaji na ziara za mara kwa mara za Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Kafulila na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, Msoleni Juma Dakawa ndizo sababu zilizochangia kuiwezesha Halmashauri ya Meatu kwa mara ya kwanza kushika nafasi ya pili kitaifa katika ukusanyaji wa mapato huku Mkoa wa Simiyu nao ukishika nafasi ya pili kitaifa.

 

Mpina amesema hayo jijini Dodoma baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Mhe. Ummy Ali Mwalimu kuitangaza Halmashauri ya Meatu kushika nafasi ya pili kitaifa  kwa mara ya kwanza kati ya kundi la  Halmashauri za wilaya 137 nchini  na kufanikiwa kukusanya asilimia 51 ya malengo katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2021.

 

Waziri Ummy pia aliutangaza Mkoa wa Simiyu kuwa umeshika nafasi ya pili kitaifa kwa kuweza kukusanya asilimia 35 ya lengo katika kipindi cha robo mwaka kuanzia Julai na Septemba mwaka huu

 

Mpina ameitaja sababu nyingine zilizowezesha Halmashauri ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kupata mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuzibwa mianya ya uvujaji mapato na kuchukua hatua kali kwa wabadhilifu wa fedha za umma.

 

Hivyo mafanikio hayo yatawezesha fedha zinazopatikana kutumika vizuri kuleta maendeleo ya wananchi na kutimiza malengo ya Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla.

 

Mpina amesema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila tangu aingie katika mkoa huo kila mwezi anatembelea wilaya zake zote maeneo ya kazi, kufanya mikutano ya hadhara na kutatua kero za wananchi.

 

Pia amekuwa akisimamia na kufuatilia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuhakikisha yanakusanywa kwa usahihi na kuingizwa kwenye mifumo ya Serikali.

 

Mpina amesema Kafulila amekomesha ufujaji wa mapato kama ilivyokuwa imezoeleka siku za nyuma na kuwachukulia hatua wote waliozoea kudokoa fedha za umma

 

 

 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Kafulila (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meatu, Juma Mwiburi wakati wa ziara yake ya kukugua shughuli za ukusanyaji mapato yatokanayo na mazao ya uvuvi katika Ziwa Eyasi katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Kafulila akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sakasaka wilaya ya Meatu alipokwenda kusikiliza na kutatua kero zao pamoja na kufuatilia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Zacharia Kafulila akizungumza na wananchi wa Kata ya Kaloleni wilaya ya Busega kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kufuatilia ukusanyaji mapato ya Serikali.kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Gabriel Zacharia.

 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Zacharia Kafulila akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwaukoli Wilaya ya Meatu kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero zao pamoja na ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments