KAMPUNI YA SUKARI YA KAGERA YAONGOZA KATIKA MKOA WA KAGERA KATIKA UWASILISHAJI MICHANGO NSSF

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na watendaji wa kiwanda cha sukari Kagera alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Kanali Wilson Sakulo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wahandisi wa kilimo wanaofanyakazi katika Kiwanda cha Sukari Kagera, alipotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Kulia ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif na kushoto ni Mbunge wa Nkenge, Mhe. Florent Kyambo.

 

Na Mwandishi Wetu, Kagera


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuongeza uwekezaji hivyo kazi kubwa ya Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi ili wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wasikwame.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelea kiwanda cha sukari Kagera kwa ajili ya kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa pamoja na kukagua shughuli za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) zinazofanywa kiwandani hapo ikiwemo uwasilishwaji wa michango.

Waziri alisema Serikali inataka kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kiwanda hicho cha sukari Kagera unakwenda mbele kwa faida ya Tanzania, lengo ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa sukari na pia iweze kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi na kupata fedha za kigeni.

Alisema kiwanda cha sukari Kagera licha ya kutengeneza ajira nyingi kwa vijana, lakini ndiye mwajiri namba moja anayeongoza kwa mkoa wa Kagera kwa kupeleka michango ya wafanyakazi wake wapatao takribani 8,000 ambapo kila mwezi kinachangia zaidi ya Shilingi milioni 540 NSSF.

“Huyu ndiye mwekezaji mwenye wanachama wengi NSSF kwa mkoa wa Kagera na pia ni mchangiaji mzuri wa michango ya wanachama wake, nitoe wito kwa waajiri wengine waige mfano wa mwekezaji huyu kwa kulipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati,” alisema.

Waziri Jenista alisema kazi kubwa ya NSSF ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao hivyo fedha za michango zinazokusanywa na NSSF zinaenda kuwekezwa kwenye miradi mingine ndani ya nchi ambayo inasaidia kukuza uchumi wa Taifa.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora aliipongeza  NSSF katika mkoa huo kwa kuweza kupunguza kero za wanachama na wadau kwa asilimia zaidi ya 90 kutokana na muda mrefu sasa uongozi wa mkoa huo haujapokea malalamiko yoyote ya wanachama wa NSSF.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cosmas Sasi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba, alisema kiwanda cha sukari cha Kagera kwa upande wa NSSF ni mdau mkubwa kwani kina wanachama wengi.

Mbunge wa Nkenge, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Mhe. Florent Kyambo, alisema mwekezaji huyo licha ya kutengeneza ajira kwa Watanzania, lakini ni mlipaji nzuri wa michango ya wafanyakazi wake NSSF.

Naye, mwekezaji wa kiwanda cha sukari Kagera, Seif Seif alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kuwa na dira ya kukuza viwanda vya ndani na kuweza kuvilinda ili viweze kukua.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Mhandisi Atugonza Phinis ambaye ni mwendeshaji mitambo kiwandani hapo, alisenma kampuni ya Kagera imekuwa ikitoa ajira nyingi kwa vijana na kwamba wanafurahishwa na namna mwekezaji huyo anavyojali maslahi ya wafanyakazi wake kwa kuwapelekea michango NSSF ili pale watakapopatwa na janga waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments