AMUUA MKE KWA PANGA AKIMTUHUMU KUCHEPUKA..AJISALIMISHA MWENYEWE POLISI KAHAMA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Tuesday, October 5, 2021

AMUUA MKE KWA PANGA AKIMTUHUMU KUCHEPUKA..AJISALIMISHA MWENYEWE POLISI KAHAMA


Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Marco Maduhu, Shinyanga
Mwanamke ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mbulu Kata ya Mhongolo Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Regina Jiyenze (45) amedaiwa kuuawa na mume wake Heneriko John(53) kwa kumkata mapanga kichwani na mabegani, kisha kujisalimisha Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo limetokea leo Jumanne Oktoba 5,2021 majira ya saa tatu asubuhi katika Mtaa wa Mbulu Kata ya Mhongolo Manispaa ya Kahama.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa sio mwaminifu kwenye ndoa yao, kitendo ambacho kilimfanya mtuhumiwa kujichukulia sheria mkononi na kumkata mapanga na kusababisha kifo chake.

“Eneo la tukio tumeokota panga lenye damu likiwa umbali wa mita 20 kutoka katika eneo la tukio lilipotendeka, mtuhumiwa tunamshikilia mara baada ya kujisalimisha mwenyewe, na tutamfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika,”alisema Kyando.

“Mbinu iliyotumika ya kumkata mapanga mke wake ni kumvizia marehemu wakati akiwa nyumbani kwa balozi Manungu Bundala, alipofika kwa ajili ya kushtaki kutishiwa kuuawa na mume wake, ndipo alipokatwa mapanga sehemu za kichwani na mabengani na kufariki dunia,”aliongeza.

Pia Kamanda  Kyando alitoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, kisa wivu wa mapenzi, kwani kitendo hicho hakifai na kinaonekana kimekuwa sugu, huku akitoa ushauri kwa wapenzi au wanandoa kuwa wakiona mwenzake sio mwaminifu kwenye mahusiano waachane, ambapo wataingia kwenye matatizo kujutia kwenye maisha yao.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages