AJALI YA BASI YAUA WATU WANNE KUJERUHI 33 KAGERA


Watu wanne wamethibitika kupoteza maisha na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Fikoshi lililokuwa likitoka Mkoa wa Mwanza kuelekea mkoa wa Kagera kuacha njia na kupinduka katika mteremko wa Nyangoye uliopo katika Manispaa ya Bukoba Mkoa wa Kagera.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali amesema kuwa, basi hilo lenye namba za usajili T710 BXB wakati linapata ajali lilikuwa likitokea Mkoa wa Mwanza na lilikuwa limebakiza umbali mfupi kuingia katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Bukoba.


"Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali na idadi ya abiria waliokuwemo, tunaomba subira taarifa rasmi itatolewa baadae ikikamilika," amesema.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amethibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha watatu ni watu wazima na mmoja ni mtoto mdogo.

Kamanda huyo amesema miili ya marehemu imepelekwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera na majeruhi wamepelekwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.

Amesema uchunguzi unaendelea na taarifa za watu walioshuhudia wamedai gari hilo lilipoteza mwelekeo baada ya kumaliza kona katika mteremko huo na kuanguka pembezoni mwa barabaraba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments