BASHUNGWA AIPONGEZA TAIFA STARS KUICHAPA MADAGASCAR 3 - 2, ATOA ZAWADI YA MILIONI 10


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amewapongeza vijana wa Timu ya Taifa Stars na Watanzania wote kwa ushindi wa Magoli 3 - 2 dhidi ya Timu ya Madagascar kwenye mchezo uliochezwa leo Septemba 07, 2021 wa Michuano ya Kufuzu Kombe la Dunia 2021.

Bashungwa ameeleza kuwa Wizara itawapa zawadi ya Tsh 10,000,000/=  kuwapongeza kwa jitihada safi ya mapambano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2021.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa kuwaomba wadau wowote wenye zawadi kwa Taifa Stars wawasiliane na Wizara ili kutambua zawadi ya michango hiyo ya hamasa kwa Taifa Stars.

Timu ya Taifa ya Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Madagascar katika mchezo wa Kundi J kufuzu Kombe la Dunia uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana 2-2, Taifa Stars ikitangulia kwa mabao ya kiungo wa Simba SC ya nyumbani, Erasto Edward Nyoni dakika ya tatu tu kufuatia mshambuliaji wa Wydad Athletic ya Morocco, Simon Happygod Msuva kuangushwa kwenye boksi.

Kiungo wa Maccabi Tel Aviv ya Israel, Novatus Dismas Miroshi akaifungia bao la pili Taifa Stars dakika ya 26 akimalizia kazi nzuri ya Nahodha na mshambuliaji wa Royal Antwerp ya au Ubelgiji, Mbwana Ally Samatta.

Madagascar ikazinduka kwa mabao ya winga wa Suphanburi FC ya Thailand, Njiva Tsilavina Martin Rakotoharimalala dakika ya 36 na beki wa Lorient ya Ufaransa, Thomas Fontaine dakika ya 45 na ushei.
Na shujaa wa Taifa Stars leo amekuwa kiungo wa Yanga SC ya nyumbani, Feisal Salum Abdallah aliyefunga bao la ushindi dakika ya 52.
Kwa ushindi huo, Tanzania inapanda kileleni Kundi J ikifikisha pointi nne baada ya mechi mbili, kufuatia sare ya 1-1 na wenyeji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kwanza Alhamisi iliyopita.
Benin inafuatia ikiwa na pointi nne pia, wakati DRC ni ya tatu kwa pointi zake mbili na Madagascar hawana pointi baada ya kufungwa nyumbani na ugenini mfululizo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments