WADAU DODOMA WAKUTANA KUJADILI UHAMASISHAJI NA UTOAJI ELIMU YA SENSA YA WATU NA MAKAZI





Na Dotto Kwilasa, Dodoma

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewakutanisha  viongozi wawakilishi wa Serikali ngazi mbalimbali,makundi ya kijamii ,Taasisi za dini,Umma ,binafsi na vyama vya siasa katika kikao cha pamoja kwa lengo la uhamasishaji na utoaji wa elimu ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 .

Akieleza umuhimu wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka amesema wameandaa kikao hicho na kuyashirikisha makundi hayo ili kurahisisha utoaji wa elimu ya sensa kwa jamii huku akisisitiza kwamba kwa kufanya hivyo zoezi hilo litafanikiwa kama inavyotarajiwa.

Kwa kutambua umuhimu wa zoezi hilo, Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene  amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi katika zoezi  la  sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwakani  ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo na kukuza uchumi.

Akiongea katika  kikao hicho amesema “Serikali inategemea sana zoezi hili,hatuwezi kuwa na maendeleo bila kujua idadi ya watanzania,kila mmoja kwa nafasi yake anatapaswa kuwa balozi wa uhamasishaji  ni muhimu hivyo watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuisaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo”.

Mbali na hayo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Antony Mtaka  kwa kuona haja ya kuandaa mkutano huo huku akisisitiza kwamba sensa ni muhimu kwani inaleta ushahidi wa kisayansi na maendeleo.

Naye Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Job  Ndugai amesema zoezi hilo ni muhimu kwa Taifa kwani litasaidia Nchi kupanga maendeleo hivyo watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

“Tarehe 31 vikao vyetu vya Bunge vitaanza na vikao vilivyopita tumepitisha mambo mengi ikiwemo na tozo,safari hii itakuwa salama,hili ni jambo muhimu sana hivyo niwaombe watanzania wajitokeze kwa wingi,sisi wagogo hata zoezi la kuhesabu mifugo linakuwa na shida ni utamaduni wetu,”amesema.

Naye Kamisaa wa Sensa nchini ambaye pia ni Spika wa Bunge Mstaafu,Anne Makinda ametoa wito kwa watanzania kujitokeza katika zoezi la kuhesabiwa kwani hilo sio suala la kisiasa na kwamba  zoezi hilo watatumia tehama katika maeneo ya kuhesabiwa lengo likiwa ni kuwafikia watanzania wengi ambapo amedai watawafikia watu wengi mpaka katika maeneo ya vijijini.

Makinda amesema wamejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi  kwani kwa sasa wataaalamu wameongezeka tofauti na miaka ya nyuma.

Kutokana na hayo Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema Serikali imejipanga kikamilifu  kusimamia  zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa  kufanyika mwakani huku akitoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi hilo.

“Sensa hii itakuwa ni ya sita itasimamiwa na Serikali ya awamu ya sita kwa weledi  mkubwa tunatarajia watahesabiwa zaidi ya watu milioni 64 kwani kila mwaka watu wanaongezeka milioni 3.1 na sensa mwisho ya mwaka 2012 tulikuwa milioni 49,”amesema.

Amesema kwa sasa wanauzoefu wa kutosha na wamejipanga kuhesabu watu mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu ambapo ambapo amedai zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria hivyo ni lazima watu wahesabiwe.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bill Chidabwa ameiomba Ofisi  ya Taifa ya Takwimu (NBS)  kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kuhesabiwa katika zoezi la  sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani  ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo na kukuza uchumi.

Amesema wao vijana wanaunga mkono zoezi hilo ambapo ameitaka pia NBS mara baada ya zoezi hilo kuja na majibu vijana wapo wangapi na wanatakiwa kupewa kipaumbele kwa kaisi gani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments