WATATU WAKAMATWA WAKIJIFANYA MAOFISA WA TANESCO ARUSHA


Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo

Na  Abel Paul Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia vijana watatu wenye umri kati ya miaka 20 hadi 26 wakazi wa mkoani humo kwa kosa la kuwadanganya wananchi wanaohitaji kuunganishiwa umeme kwamba wanaweza kuwapatia huduma hiyo kwa njia ya mkato kwa kuwa wao ni maofisa wa TANESCO.

Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 18, 2021, na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo  na kusema kwamba watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 17, 2021, katika ofisi za TANESCO zilizopo Mtaa wa Old Line, Kata ya Themi, Halmashauri ya Jiji la Arusha.

"Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifanikiwa kuwakamata watu watatu ambao ni Gidioni William (26) mkazi wa Sombetini, Richard Frank  (20) Mkazi wa Daraja la II, Godson Erick  (20) Mkazi wa Moshono wakijifanya watumishi wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Arusha.

"Watuhumiwa hao walikamatwa mara baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa toka kwa raia wema kwamba, wamekuwa wakijihusisha na wakuwadanganya wananchi ambao wanahitaji huduma za kuunganishiwa umeme kuwa wao ni Maofisa wa Shirika hilo na wana uwezo wa kuwapatia huduma wanazozihitaji kwa njia ya mkato, ndipo timu ya makachero wa Polisi wakishrikiana na maofisa wa shirika la Umeme waliweka mtego na kufanikisha kuwakamata watuhumiwa hao",amesema Kamanda.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha amesema kutokana na tuhuma hizo Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linaendelea kuwahoji watuhumiwa ili kupata mtandao mzima unaohusika na vitendo hivyo vya kitapeli katika ofisi za shirika la umeme (Tanesco) Mkoa wa Arusha.

Ameeleza kuwa pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuzitumia ofisi na taasisi za umma ambazo zipo kwa ajili yao pindi wanapohitaji huduma yoyote hali hii itasadia kuwakwepa walaghai ambapo wanaweza kuwaingiza katika matatizo au hasara.

Aidha amewaomba wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post