WAZIRI MKUU : SERIKALI IMETUMIA SH. BILIONI 172.644 KULIPA MADENI YA WATUMISHI WA UMMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kassim Majaliwa

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

SERIKALI imesema,katika kipindi cha Mei 2021 hadi sasa imetumia jumla ya Sh. bilioni 172.614 kulipa madeni mbalimbali  ya watumishi wa umma na inaendelea kulifanyia kazi suala hilo ili lisiendelee kuwa kero kwa wastaafu katika kumudu maisha baada ya kustaafu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema hayo leo (Jumatano, Agosti 25, 2021) Jijini hapa Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa nane wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa(TALGWU). 

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) uhakikishe unatumia fedha na rasilimali za chama hicho kwa kuwahudumia wanachama wao wote bila ubadhirifu.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanaTALGWU na kuwasihi waendelee kushirikiana, kushikamana na kuwajibika kwa kuzingatia uadilifu kwani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ni silaha kuu katika kufikia malengo ili kupunguza mzigo kwa Serikali.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi watakao fanikiwa kuibuka kidedea katika uchaguzi watakaoufanya leo wahakikishe wanaenda kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa weledi mkubwa na kwa kuweka maslahi ya wanachama wao mbele. 

Amesema hadi sasa zipo halmashauri 18 ambazo hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi, hivyo amemuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama kuwaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe mabaraza hayo yanaundwa ifikapo ama kabla ya tarehe 30 Septemba 2021.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19, Waziri Mkuu amewataka wananchi wafuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujinga na ugonjwa huo na pale wanapoona dalili ambazo hawazielewi wawahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu.

 “Kama mnavyofahamu, kuwa dunia nzima ipo kwenye wimbi la tatu la UVIKO 19. Janga hili lipo nchini na limesababisha baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kuendelea kuugua. Kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.”

Amesema kuwa chanjo ya UVIKO 19 inapatikana na inasambazwa nchini kote ikiwemo hapa Dodoma ambapo huduma hiyo inatolewa katika vituo 89 ndani ya mkoa. “Sambamba na vituo hivi, pia ipo huduma ya mkoba (mobile) ambapo watumishi wa afya wanakwenda katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo makampuni ya ujenzi na kutoa huduma”

“Niwatoe hofu wananchi wote kuwa chanjo hii ni salama, haina madhara yoyote na ni hiyari na hakuna atakayechanjwa pasipo ridhaa yake. Hivyo, niwaombe wananchi kujiepusha na watu wanaopotosha ukweli kuhusu suala la chanjo.”

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa TALGWU  ni chama imara miongoni mwa vyama vya wafanyakazi nchini na kwamba uongozi wa chama hicho  ni imara na unazingatia katiba,  kanuni na miongozo katika kuwatumikia wanachama wake.

Ametumia nafasi hiyo pia kuvikumbusha vyama vya wafanyakazi ambavyo bado havijakamilisha taratibu za uchaguzi kwa mwaka huu kufanya hivyo maramoja ili kuendana na muda uliopangwa kabla ya mwezi wa 11  haujaisha.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashidi Mtima amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuchukua hatua madhubuti zenye lengo la kuondoa kero na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post