MWANAMKE ABAKWA, AUAWA KISHA KUTUPWA VICHAKANI, MWINGINE AKATWA SHINGO PWANI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) sare za jeshi hilo zilizokamatwa kwa mtuhumiwa Otto William ambaye alikuwa akitumia kufanyia uhalifu,sare hizo zimekamatwa kufuatia msako mkali uliofanyika katika kipindi cha siku 10.(Picha na Rotary Haule).

Na Rotary Haule, Kibaha

WATU watatu wameuawa kikatili katika matukio tofauti yaliyotokea sehemu mbalimbali mkoani Pwani likiwemo la mwanamke mmoja kubakwa kisha kuuawa na mwili wake kutelekezwa vichakani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,Wankyo Nyigesa amewaambia waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa, tukio la kwanza lilitokea Agosti 8,mwaka huu saa 9 jioni katika Kitongoji cha Tobora Kata ya Msata Chalinze mkoani Pwani.

Wankyo amesema katika tukio hilo mwanamke mmoja (26) Mkazi wa Pongwe Msungura alibakwa kisha kuuawa na kisha mwili wake kutelekezwa vichakani,lakini mtuhumiwa mmoja amekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku Jeshi la Polisi linaendelea kumhoji.

Katika tukio la pili Kamanda Nyigesa,alisema kuwa mwanamke mwingine ambaye jina lake limehifadhiwa Mkazi wa Kijiji cha Kitonga Wilayani Bagamoyo aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni kisha kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Nyigesa,alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 4 mwaka huu saa 12 jioni huko katika Kijiji cha Kitonga ambapo marehemu alivamiwa shambani kwake na watu wasiojulikana na hivyo kutekeleza mauaji hayo.

Aidha,katika tukio la tatu mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Kwarohombo Kata ya Mbwewe Chalinze ambaye jina lake halijafahamika aliuawa kwa kupigwa mkuki na wafugaji ambapo hata hivyo Jeshi la Polisi lipo katika msako dhidi ya wahalifu hao.

Katika tukio jingine Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Sijali Idd akiwa na Gobole moja ,unga wa baruti na gololi 11zinazotumika katika Gobole hilo.

Kamanda Nyigesa,alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 4 mwaka huu saa 11 jioni katika Kijiji cha Msimbani Kata ya Miono Wilayani Bagamoyo.

Nyigesa,alisema imebainika kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia silaha hiyo kufanya shughuli za uwindaji kinyume na utaratibu lakini atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Wakati huo huo Jeshi hilo limemkamata Otto William (28)Mjaluo mkazi wa Kibondeni Kibaha akiwa na sare za Jeshi la Polisi ambazo (Khaki) General Duty pea 3,Mkanda wa bendera 1,Mkanda wa JKT 1,Ballet 1,buti pea 3 ,mbili zikiwa nyeusi na 1 ya khaki,begi la mgongoni,na Sweta.

Nyigesa ,alisema mtu huyo amekamatwa Agosti 5 mwaka huu saa 5:30 usiku huko nyumbani kwake,Kibondeni kwa Mathias Kibaha Mjini ambapo inadaiwa mtuhumiwa alikuwa anatumia sare hizo kufanyia uhalifu.

Hata hivyo, Nyigesa alitoa wito kwa wananchi kutii sheria bila shuruti na kutoa taarifa za kiuhalifu kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya dola ili wahalifu hao wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo. 

CHANZO - DIRA MAKINI BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments