AJALI YA MAGARI MATATU YAUA WATU 9 MOROGORO... MOJA LILIWEKA MASHADA YA MSIBA KUKWEPA TRAFIKI


Watu tisa wamefariki dunia na wengine 24 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu iliyotokea eneo na Nanenane mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Jumanne Juni 22, 2021.

Magari hayo ni Toyota Coaster, Cresta na lori la kampuni ya Dangote ambapo Coaster hilo lililogonga gari dogo na kisha kugongana na lori.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Coaster kutaka kulipita gari dogo na kupoteza mwelekeo.

Amesema katika ajali hiyo watu watano walifariki hapo hapo, wakiwemo madereva wa lori, Selemani Chali na Adamu Minde na abiria aliyefahamika kwa jina moja la Nassor.

"Chanzo cha ajali hiyo ni gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya likiendeshwa na Minde kutaka kulipita gari jingine aina ya Toyota Cresta lililokuwa likiendeshwa na Emmanuel Sembuche bila kuchukua tahadhari. Gari hilo liliigonga Cresta na kupoteza mwelekeo na kukutana uso kwa uso la lori hilo mali ya kampuni ya Dangote lililokuwa likiendeshwa na Chali",ameeleza Kamanda Muslim.

Amewaonya madereva wa magari kuacha kuweka maua kwenye magari ili ionekane wanakwenda msibani ili lengo likiwa kukwepa kusimamishwa na askari wa usalama barabarani.

“Lile Coaster lilikuwa na mashada ya maua wakiashiria kuwa walikuwa wanapeleka maiti ili askari wasiwakamate. Nawaonya madereva kuacha tabia kama hii, tumejipanga vizuri kuhakikisha udanganyifu kama huo hautokei tena” ,amesema Kamanda Muslim.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dkt Kessy Ngalawa amesema saa 6 usiku walipokea majeruhi na miili saba na ilipofika asubuhi vifo viwili viliongezeka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments