WALIOKAIDI MKATABA WA NARCO KIKAANGONI NDANI YA SIKU KUMI


Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa siku kumi kwa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kubaini na kuwanyang’anya maeneo, wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa ambao wamebadili matumizi ya ardhi kinyume na makubaliano ya mikataba yao.

Waziri Ndaki amebainisha hayo jana (12.01.2021) wakati alipotembelea Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kufanya mkutano wa hadhara na baadhi ya wawekezaji, wakulima na wafugaji, ambao wanafanya shughuli zao katika ranchi hiyo na kubaini kuwa baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu na NARCO kwa ajili ya kufuga na kulima malisho ya mifugo wamekuwa wakikodisha maeneo hayo kwa wakulima na wafugaji kinyume na mkataba.

“NARCO siku kumi nadhani zinawatosha kubaini watu wanaojiita wawekezaji, waliobadilisha matumizi ya ardhi ambayo siyo kufuga wala malisho wanyang’anywe maeneo kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu wa mkataba kati yao na NARCO, na mimi nitafuatilia nitapenda kupata taarifa mmepata wangapi na wangapi wamenyang’anywa kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu waliokubaliana.” Amesema Mhe. Ndaki

Waziri Ndaki amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Mbarali kuwa wamekuwa wakikodishwa maeneo ya ranchi hiyo na wawekezaji kwa shilingi elfu ishirini kwa hekari moja kwa ajili ya kilimo na madebe kumi ya nafaka baada ya mavuno kwa kila hekari moja, huku wafugaji wakilipa takriban shilingi milioni mbili kwa hekari moja katika kipindi cha miezi minne kwa ajili ya kulisha mifugo yao kwenye maeneo ya wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu na NARCO kwa mkataba wa kufuga au kulima malisho ya mifugo.

Amefafanua kuwa mkataba wa NARCO na wawekezaji kwa ajili ya kufugia mifugo na kulima malisho hauruhusu wawekezaji kukodisha eneo kwa mtu mwingine kwa ajili ya shughuli zozote kwa kuwa maeneo ya ranchi za taifa ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Kuhusu deni la zaidi ya Shilingi Bilioni Sita ambalo NARCO inawadai wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa NARCO kufikia Tarehe 15 Mwezi Februari Mwaka 2021 saa saba mchana awe amepata taarifa ya wawekezaji waliolipa madeni yao pamoja na ambao bado hawajalipa, kabla ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi.

“Wawekezaji wote ambao tunawadai hapa Usangu na kwenye ranchi zingine wote walipe pesa ya NARCO tulipokubaliana kwenye mkataba tulikubaliana mtalipa pesa, mlipe madeni yenu ifikapo tarehe 15 mwezi februari saa saba mchana muwe mmelipa madeni yenu tunataka NARCO ijiendeshe kibiashara, lakini sioni tukielekea kwenye kujiendesha kibiashara na moja ya matatizo yanayotufanya tusifike huko ni kulea watu wa namna hii.” Amefafanua Mhe. Ndaki.

 

Ameongeza kuwa wale ambao hawatakuwa wamelipa hadi kufikia muda huo wanyang’anywe maeneo hayo ili wapatiwe watu wengine ambao wataweza kulipa kwa mujibu wa mkataba ili NARCO iweze kufikia malengo yake na kulalamika kuwa NARCO imechelewa kuchukua hatua kwa watu ambao wamekuwa na madeni ya siku nyingi.    

Amesema kuwa wizara imefanya tathmini juu ya madeni hayo na kuagiza yalipwe katika viwango na tozo mpya zilizowekwa kwa sababu imejiridhisha kwamba kwa gharama hizo NARCO itaweza kujiendesha na kuhudumia vizuri ranchi zake.

Kwa mujibu wa taarifa ya NARCO iliyotolewa na Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Masele Mipawa, maeneo ya vitalu katika ranchi za taifa yanayokodishwa kwa wawekezaji yamegawanywa katika viwango vitatu, ambapo kiwango cha chini ni Shilingi 3,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta 1 hadi 2000, kiwango cha kati ni Shilingi 5,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta kuanzia hekta 2001 hadi 5000 na kiwango cha juu ni Shilingi 7,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta zaidi ya 5001.

Aidha Waziri Ndaki, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia namna ya kukodisha maeneo ya ranchi za taifa kwa wakulima ambao wanaweza kulima malisho ya mifugo ili kuondokana na migogoro ya wakulima kupata maeneo kwa ajili ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi.

Amesema ni muda muafaka kwa wizara kuangalia namna wananchi wanavyoweza kutumia maeneo hayo kwa ajili ya tija kwa taifa badala ya kusubiri wawekezaji ambao baadhi yao wamekuwa wakienda kinyume na makubaliano ya mikataba na kuwafanya wananchi wanaoishi karibu na ranchi za taifa kukosa maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema atahakikisha anasimamia maelekeo yote yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki likiwemo la wawekezaji kulipa madeni ya vitalu walivyokodishwa ili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inayomiliki maeneo hayo iweze kujiendesha kibiashara kama moja ya malengo ya kampuni hiyo kupitia maeneo yake.

Katika mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wakulima, wafugaji na wawekezaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali, Bibi Uliya Mahenge amemuomba Waziri Ndaki kuwapatia wakulima maeneo kwenye ranchi za taifa ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo huku wakilipa kodi ya serikali ya maeneo hayo watakayokidishwa kama ambavyo wafugaji wanavyopatiwa vitalu kwa ajili ya kufugia mifugo kwenye ranchi hizo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo katika ziara hiyo alikuwa na lengo la kufahamu changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu ambayo ni moja ya ranchi zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post