PENCE AKATAA KUTUMIA IBARA YA 25 KUMUONDOA TRUMP MADARAKANI


Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amemwambia rasmi spika wa bunge Nancy Pelosi kwamba haamini kuwa hatua ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya nchi hiyo kumuondoa Trump madarakani ni kwa manufaa ya nchi au hata kuendana na katiba.

Ujumbe wa Pence umejiri mnamo wakati baraza la wawakilishi lilikuwa likijadili pendekezo la kutumia ibara hiyo ya 25.

Hata hivyo inatarajiwa kuwa wabunge wataendelea na mchakato wa bunge kwa lengo la kumuondoa Trump au kuzima matarajio yake kuwania urais baadaye.

Awali katika tukio tofauti, Rais Trump alisema ibara hiyo haitakuwa na maana yoyote kwake. 

Trump alisema pia kuwa wito wa kutaka aondolewe madarakani kwa njia ya mashtaka bungeni vilevile ni baya zaidi.

Kwingineko, majenerali wakuu wa jeshi nchini Marekani, wameshutumu uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Rais Trump dhidi ya majengo ya bunge wiki iliyopita.

Kwenye taarifa ya pamoja iliyosainiwa na wakuu wanane wa kijeshi wakiongozwa na mwenyekiti wao jenerali Mark Milley, tukio hilo lilikuwa shambulizi la moja kwa moja dhidi bunge la Marekani na dhidi ya mchakato wa kikatiba.

Shirika la upelelezi FBI limesema tayari limewafungulia watu 170 mashtaka na mamia kadhaa pia watakamatwa na kushtakiwa.

Jeshi la nchi hiyo limesema litawapeleka maafisa wake wa kikosi cha ulinzi wa taifa 15,000 kushika doria siku ya kuapishwa kwa Joe Biden, Januari 20.

 

Credit:DW



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments