Vijana wa Skauti wakizibua mtaro. |
Na Dotto Mwaibale.
CHAMA cha Skauti Mkoa wa Mbeya kimetoa msaada kwa kuwasaidia waathirika wa mafuriko katika Kata ya Kalobe jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Kamishna wa Skauti wa mkoa huo Mratibu wa Majanga wa chama hicho mkoani humo, Lusajo Sanga alisema eneo lililoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni Mtaa wa Maendeleo A katika kata hiyo.
Alisema mafuriko hayo yalitokea Januari 8 mwaka huu kufuata mvua kubwa iliyonyesha.
" Eneo hilo liliathiriwa zaidi na mafuriko hayo kutokana na mifereji ya maji kuziba hivyo maji ya mvua kukosa muelekeo na kwenda kwenye makazi ya watu" alisema Sanga.
Alisema baada ya kutokea mafuriko hayo walisaidia na Kamishna wa Skauti Mkoa huo, Sadock Ntole, kuratibu namna ya kwenda eneo la tukio kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika ikiwa ni pamoja na kuchimba vyoo vilivyosombwa na maji, kuzibua mitaro na kuwafariji waathirika kwa kushirikiana na diwani wa kata hiyo na viongozi wengine.
Sanga alisema mafuriko hayo yaliathiri nyumba tano katika mtaa huo ambapo nyumba ya mkazi mmoja wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Mama Muro na Bibi Tamali Mwalukunga ziliathiriwa zaidi kwani sehemu ya nyumba yake na choo vilibomoka ambapo walilazimika kumjengea choo kingine cha muda.
Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole alisema wao kama skauti wamekuwa wakitoa msaada kwa jamii pale yanapotokea majanga ya namna hiyo hivyo baada ya kutokea mafuriko hayo walienda eneo la tukio kutoa msaada huo.