WANAWAKE IKUNGI WAOMBA HATUA KALI ZICHUKULIWE KWENYE KESI ZA UKATILI

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Justice Kijazi, akizungumza kwenye kikao kazi cha tathmini ya hali ya matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto wilayani humo jana kilichoshirikisha wanawake 120 waliokutanishwa na Shirika la SPRF chini ya ufadhili wa FCS ili kujadili namna bora ya kutokomeza matukio hayo kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) Dkt. Suleiman Muttani  akizungumza kwenye mkutano huo ulioshirikisha wanawake 120 kutoka vijiji 12 kuzunguka wilaya ya Ikungi, Singida. 

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali zilizojikita katika kuwajengea uwezo na kuwaimarisha katika mapambano dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani humo.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali zilizojikita katika kuwajengea uwezo na kuwaimarisha katika mapambano dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani humo.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali zilizojikita katika kuwajengea uwezo na kuwaimarisha katika mapambano dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani humo.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada mbalimbali zilizojikita katika kuwajengea uwezo na kuwaimarisha katika mapambano dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani humo.

Kikao kazi cha vikundi vya uhamasishaji kwa Sauti Ya Mwanamke na Sauti ya Mwanafunzi  kikiendelea.

Maafisa Watendaji wa Shirika la SPRF wakifuatilia matukio yanayoendelea kwenye kikao hicho.

Jeshi la Polisi likishiriki ipasavyo kikao hicho.

Mmoja wa waratibu wa mradi wa Aware, Bernard Maira akizungumza kwenye kikao hicho.

Mwenyekiti wa Sauti ya Mwanamke kwenye moja ya makundi ya uhamasishaji akizungumza.

Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ikungi, Beatrice Maeda akizungumza.

Kikao kikiendelea.
Moja ya kikundi cha Uhamasishaji cha Sauti ya Mwanamke wilayani  Ikungi  wakieleza moja ya tukio la ukatili wa kijinsia walilofanikiwa kuliibua.

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA lisilo la Kiserikali linalojikita zaidi katika mlengo wa shughuli za kupunguza umaskini kwa afya na ustawi nchini (SPRF) kupitia mradi wake wa  ‘Aware’ jana limewakutanisha wanawake 120 kutoka vijiji 12 vya wilaya ya Ikungi, mkoani hapa kwa lengo la kuwaimarisha kuweza kukabiliana ipasavyo na  matukio ya ukatili.

 Jumla ya matukio ya ukatili wa kijinsia 104 yameripotiwa kufanyika ndani ya Wilaya ya Ikungi  kwa kipindi cha kati ya Julai 2019 hadi Novemba 2020, ambapo kati ya matukio hayo 56 yalijitokeza katika kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020, huku matukio mengine 48 ya aina hiyo hiyo yakijitokeza  kipindi cha Machi hadi Novemba 2020.

Kwa mujibu wa SPRF chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) imebainika kuwa kati ya matukio hayo 56 yaliyoripotiwa kutoka vijiji 12 vya mradi huo kwa kipindi hicho cha Julai 2019 hadi Februari 2020 ni kesi 2 ndizo zilizofikishwa kwenye ngazi ya mahakama, na kati ya hizo kesi moja pekee ndiyo iliyotolewa hukumu.

Matukio mengine 7 ya ukatili yaliyoripotiwa yaliishia kwenye Kituo cha Polisi Ikungi kutokana na kukosa vielelezo na ushahidi shawishi, huku kesi 4 zikikomea kwenye vituo vidogo vya polisi, 7 kwenye ngazi za kata, 16 ngazi ya vijiji, 5 ngazi ya vitongoji na 14 zikiishia kutatuliwa kindugu kwenye ngazi ya familia.

Aidha, kwa upande wa matukio 48 yaliyojitokeza  kwenye kipindi cha Machi hadi Novemba 2020 ni kesi 2 pekee ndizo zilizofikishwa na kuamriwa kwenye ngazi ya mahakama, huku matukio mengine 11 yakiishia Kituo cha Polisi Ikungi, 5 vituo vidogo vya polisi kwenye maeneo hayo, 1 ngazi ya kata, 12 vijiji, 6 Ustawi wa Jmii Wilaya, 2 Vitongoji na  7 zikiishia kutatuliwa kindugu kwenye ngazi ya familia.

Wakichangia ripoti hiyo kabla ya kufikia maazimio, baadhi ya wanawake kutoka kwenye majukwaa ya Sauti za wanawake na Sauti za Wanafunzi wilayani hapo walisema bado kuna udhaifu mkubwa katika kushughulikia utekelezaji wa sheria zinazopinga  vitendo vya ukatili.

“Suala hili limeendelea kuwa sugu na linalochochea  ongezeko la matukio ya kufedhehesha, undugu, ujamaa na urafiki ndio chanzo kikubwa kinachoathiri mwenendo wa mashauri haya ya ubakaji, ndoa za utotoni na mimba za umri mdogo hasa pale tunaporuhusu yamalizwe kwenye ngazi za familia,” alisema mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Anna Heneriko.

Mwingine Pili Hussein alisema kesi nyingi zimekuwa zikimalizwa kwenye ngazi ya vituo vya polisi na kwa maaafisa watendaji. Lakini kubwa zaidi kuna uvujishaji mkubwa wa siri kwa watoa taarifa jambo ambalo linafifisha hamasa ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo. 

Kupitia mkutano huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justice Kijazi aliwataka maafisa wa ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria katika kuhakikisha mashauri yote yanayoripotiwa yanafikishwa kwenye ngazi za utatuzi wa kisheria.

“Niwahakikishieni mama zangu wote mliopo hapa serikali yenu chini ya Rais John Pombe Magufuli ni sikivu sana, na inakwazwa sana na aina yoyote ya uhalifu na uvunjifu wa sheria kwa makusudi. Nimeguswa sana na matukio haya yanayofedhehesha mama zetu na watoto wetu…chukueni namba zangu za simu ili yeyote kati yenu atakayeona tukio lolote la ukatili likitendeka anijulishe,” alisema Kijazi

Aidha, Kijazi aliwataka aliwataka maafisa Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanashughulikia kikamilifu kesi za matukio yote ya ukatili yanaripotiwa kwa utimilifu unaozingatia matakwa ya kisheria kwa minajiri ya kutokomeza kabisa vitendo hivyo, sambamba na kuwezesha haki kuonekana kutendeka.

 Hata hivyo, Jeshi la Polisi Ikungi kupitia mkutano huo liliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha pindi matukio hayo yanapojitokeza, na hasa kutoharibu wala kuwashawishi wahanga kuficha ushahidi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe pindi matukio hayo yanapojitokeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF, Dkt. Suleiman Muttani  alisema lengo la kikao hicho ni kutaka kuyaimarisha kiutendaji majukwaa ya vikundi vyote vya uhamasishaji dhidi ya matukio ya ukatili, ikiwemo kundi la Sauti ya Mwanamke katika kuendelea kushirikiana na majukwaa mengine kutetea haki za wanawake na watoto.

“Azma ya mradi huu wa ‘Aware’ ni kuona mifumo ya serikali za mitaa imeimarika kwa kupokea na kuitikia kwa haraka utekelezaji wa mahitaji ya jamii hasa matakwa ya wanawake, watoto na makundi mengine athirika kuona wanatambua suala la ukeketaji, ndoa za utotoni, ukatili kwa wanawake na unyanyasaji kwa watoto haukubaliki,” alisema Muttani 

mpaka sasa kati ya matukio yote hayo yaliyoibuliwa kwa ushirikiano wa majukwaa yake mbalimbali ikiwemo Sauti ya Mwanamke, Sauti ya Mwanafunzi, Kamati za Mtakuwa na Wanaume Washawishi ndani ya Vitongoji na Vijiji ni kesi 48 pekee ndizo zilizofika kwenye ngazi za utatuzi huku nyingine utatuzi wake ukiishia kwenye ngazi za familia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post