SERIKALI YA TANZANIA, KENYA YAOMBWA KUSHIRIKIANA KUKOMESHA UHALIFU..MBUNGE WAITARA ACHANGIA MIL.5 UJENZI KITUO CHA POLISI

Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na wananchi kata ya Itiryo. Picha na Dinna Maningo

Mbunge Waitara akisalimiana na wazee kata ya Itiryo

Na Dinna Maningo,Tarime
Wananchi kata ya Itiryo wilayani Tarime mkoani Mara kwa kushirikiana na Mbunge wao wa jaimbo la Tarime vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mwita Waitara wameamua kuchanga fedha na nguvu kazi ili kujenga kituo cha polisi kufuatia kuwepo kwa vitendo vya mauaji na uhalifu vinavyodaiwa kusababishwa na watu kutoka nchi jirani ya Kenya kwa kushirikiana na baadhi ya Watanzania waishio mpakani.

Mbunge huyo amedai kuchukizwa na vitendo vya mauaji na uhalifu vikiwemo vya watumishi wa serikali kuvamiwa na kuporwa fedha na mali na kudai kuwa vinamchukiza ambapo aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua waovu ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

"Tukio la mwalimu kuuwawa liliteta taswira mbaya na nilitumia nguvu nyingi kulishughulikia lakini bado watu hawasikii wanaendelea kuua na kuchukua mali za watu,kuna mwananchi wakijiji cha Itiryo alipigwa risasi akafa, na inaelezwa kuwa majambazi wanatoka nchi jirani ya Kenya na wanashirikiana na waharifu kutoka kata ya Itiryo",alisema Waitara.

Waitara alisema kuwa kuwepo kwa matukio hayo yamewapa hofu watumishi wa serikali wakiweo waalimu wa shule ya msingi Itiryo kuomba uhamisho ili kunusuru maisha yao jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma taaluma ya wanafunzi.

"Nimeambiwa kuwa kuna walimu wanataka kuhama matukio kama haya yanashusha heshima ya kabila letu la wakurya na ndiyo maana tunachukuliwa kama ni watu wakorofi,kwanini tuwafiche wahalifu lazima tuwataje kwa njia zozote hata kama ni kwa siri ili wakamatwe,tukiyaacha haya maovu watu watahama kata na uchumi utashuka, kwakuwa mmekubali kituo kijengwe nachangia milioni tano ya ujenzi",alisema Waitara.

Marwa Chacha alisema kuwa tukio la mauaji lililotokea Januari, 1/2021 na wananchi kupigwa na kunyang'anywa fedha liliondoa imani kwa wananchi na kwamba licha ya mkutano kufanyika na wananchi kuwataja waharifu lakini hawajachukuliwa hatua.

Nchagwa Matare alisema kuwa suala la kujengwa kituo cha polisi lilishazungumzwa na kuna maeneo yapo ambayo yanaweza kutumika kujenga kituo kikubwa cha polisi na kuwaomba viongozi wa serikali za vijiji kuhamasisha wananchi kuchangia fedha na nguvu kazi ili kujenga kwakuwa kitasaidia kuhimarisha usalama na kudhibiti matukio ya uhalifu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Itiryo Chacha Paulo aliwataka wananchi kuwa wavumilivu kwa kuwa suala la watuhumiwa wa uhalifu linashughulikiwa na serikali nakwamba kuna siri zingine si mpaka wananchi kuharifiwa bali ni za kiuchunguzi.

"Kata yetu imepakana na kijiji cha Gwitembe na Ntimaro ambavyo viko nchi jirani ya Kenya, tukio la siku ya mwaka mpya usiku saa tano majambazi wanaodaiwa kutoka Kenya kwa kushirikiana na wa hapa kwetu walivamia sehemu nyingi wakamuua Mohono Gasaya akiwa kwenye grosari ya mwalimu Chris na kupora fedha kwa watu wengine waliokuwa kwenye Grosari hiyo kisha wakaondoka na kuvamia nyumba ya Wankyo Meko ambako watumishi ambao ni walimu wamepanga.

"Wakiwa na lengo la kupora fedha kwa mama huyo wakachukua fedha zake laki tatu na kuchukua simu ya mwalimu Lazaro,wakaondoka na kuvamia grosari ya Mseti Magabe wakapora fedha shilingi 380,000/= na kuwapiga wateja kwa ubapa wa panga,kisha wakaelekea barabara ya inayokwenda Kenya wakakuta duka la dawa la mtumishi wakavamia n akuwaweka chini watu waliokuwepo wakachukua dawa na mteja mwingine wakamtoa simu inayotumika kusajili watu wa bima NHF na wakaondoka kwenda Kenya"alisema Paulo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa polisi walifika lakini hawakufanikiwa kuwakamata na kwamba anaiomba serikali ya Tanzania na Kenya kushirikiana ili kuwakaabili waharifu ambao wamekuwa wakifanya matukio na kukimbilia kwenye maficho ya Kenyamang'ari-Ntimaro,migodi midogo midogo ya Kehancha,Nairobi na Mombasa nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania wanakimbilia katika maficho ya misitu mkoani Morogoro.
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na wananchi kata ya Itiryo
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na wananchi kata ya Itiryo
Wananchi wa kata ya Itiryo wakimsikiliza mbunge wao Mwita Waitara
Wananchi wa Itiryo wakinyoosha mikono juu kuunga ushirikiano kati yao na serikali kuwafichua wahalifu
Wananchi wa kata ya Itiryo wakimsikiliza mbunge wao Mwita Waitara
Mwananchi akitoa kero zao juu ya matukio ya uhalifu yanayofanyika kwenye kata hiyo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post