MAABARA YA TMDA KANDA YA ZIWA YAJIIMARISHA ILI KUWA KITOVU CHA UCHUNGUZI WA VIPUKUSI



Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Kanda ya Ziwa (TMDA) Kanda ya Ziwa, Sophia Mziray.
Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA -Kanda ya Ziwa) Bugusu Nyamweri.
Mchunguzi wa Maabara ya TMDA – Kanda ya Ziwa, Maximilian Rwezaula.
Muonekano wa jengo la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya Ziwa. 

.................................................

Kaimu Mkurugenzi wa Maabara  ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA -Kanda ya Ziwa) Bugusu Nyamweri amesema TMDA inataka  maabara hiyo ibobee kwenye uchunguzi wa vipukusi, ‘Hand Sanitizers’.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA – Dar es Salaam) imeona ni vema maabara hii (TMDA – Kanda ya Ziwa) ipewe kazi hiyo kwa sababu ina vifaa vya kisasa pamoja na wachunguzi ambao wana ujuzi katika kuchunguza vipukusi Amesema Nyamweri.

Amesema maabara hiyo  itachunguza pia vipukusi vingine kwa mfano dettol, vidonge vya Chroline ambavyo huyeyushwa kwa kiwango kinachoelekezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya matumizi kwenye maeneo ya hospitalini.

Anaongeza kuwa hii ni sehemu ya vipukusi, ndiyo maana katika  mlolongo wa kuwa na vifaa vya kisasa  vya uchunguzi wa vipukusi, tumeleta mashine ya ‘Steam Distillation Unit’ ambayo ni miongoni mwa mashine zilizopo hapa maalum kwa uchunguzi wa Vipukusi.

Nyamweri anasema hii ni maalum kwa uchunguzi wa vipukusi aina ya vitakasa mikono ‘Hand Wash Sanitizers’.Vitakasa mikono ni aina mojawapo ya vipukusi (Antiseptic) ambavyo vipo katika kundi la kuua vimelea vya bakteria au vimelea vinavyosababishwa na virusi.

Akifafanua zaidi Kaimu Mkurugenzi wa Maabara hiyo Bw. Bugusu Nyamweri  anasema tulifanya uchunguzi kwa kutumia kifaa kingine lakini mashine hii ya sasa ni nzuri kwa sababu inarahisisha kazi, katika utumiaji ni nzuri katika  kutoa (kuchuja) kiwango cha pombe kinachohitajika katika sampuli ili kukamilisha uchunguzi,” anasema Nyamweri.

Anasema pamoja na uchunguzi wa kiwango cha pombe pia wanachunguza kiwango cha ‘PH’ ndani ya vipukusi hususan vitakasa mikono kwani kisipokuwa cha kutosha huweza kuathiri ngozi ya binadamu.

Anasema haimaanishi mashine ya awali haikuwa na ufanisi, ilikuwa nao, ila kutokana na  (uhitaji wa sasa), mashine hii ya sasa ni nzuri zaidi na inarahisisha kazi.

Bugusu Nyamweri anasema mashine hiyo hufanya kazi kwa dakika nne kuchuja kiwango cha ‘Alcohol’ wanachohitaji kukichunguza na kwamba ndani ya dakika sita tayari mtaalamu anakuwa ameweza kupata majibu ya sampuli yake.

“Ingawa mashine tulizokuwa tunazitumia awali zenyewe zinatumia muda mrefu katika uchunguzi, hii ya hapa Mwanza, ni ya kisasa zaidi inatoa majibu ndani ya dakika nne,” anabainisha.

Nyamweri anasema wateja wengi wanaowapokea wanaohitaji kufanyiwa uchunguzi wa vitakasa mikono wanavyotengeneza ni wajasiriamali, vituo vya afya na hospitali mbalimbali ikiwamo ile ya Kanda (Bugando) na hata vyuo vya mafunzo ya afya.

“Hii ni bidhaa muhimu ndiyo maana tunaendelea kuboresha uchunguzi wa vipukusi, kwa sababu  vinatumika mno hospitalini hivyo lazima tufuatilie kujua ubora wake, ili kuendelea kulinda afya ya jamii,” anasema.

Anasema uchunguzi wa vipukusi haukuwa katika viwango vinavyohitajika, kuna vingine ubora wake au utumiaji wake haufuatiliwi vizuri, kwa mfano kuna vile ambavyo  inabidi ‘wazimue’ na maji ili kuvitumia kwa mfano kusafisha viti meza mabenchi ya kukalia, vidonda, kuta na vifaa tiba vinginevyo.

Nyamweri anasisitiza kuwa “Tayari mipango mikakati imeshaandaliwa ikiwamo ya kuwajengea uwezo wataalamu katika matumizi ya teknolojia mpya pamoja na kuendelea kuongeza vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa vipukusi.

Anasema kwa upande wa mashine ya ‘Steam Distllation Unit’ iliyonunuliwa miezi minane iliyopita wamefanikiwa kufanya uchunguzi wa sampuli za vitakasa mikono zaidi ya 90.

“Tumeona ufanisi wa utendaji kazi wa mashine upo vizuri kwa sababu tunapima kwa kutumia  (Viwango) vya Kimataifa, inafanya kazi vizuri.

Akiielezea mashine hiyo Mchunguzi wa Maabara ya TMDA – Kanda ya Ziwa, Maximilian Rwezaula anasema mashine hii ya ‘Steam Distillation Unit’ ina uwezo wa kutathmini na kuangalia ubora wa kiwango cha pombe (Alcohol) kilichomo kwenye kitakasa mikono.

Anaongeza kuwa Inafanya kazi kwa kutumia njia ya joto ili kuondoa kiwango cha pombe kinachohitajika kwa uchunguzi kwa mvuke, ambacho hukusanywa katika kifaa maalum kisha hatua za upimaji hufanyika kwa kutumia ‘Alcohol Meter’.

Maximilian  anasema ‘Alcohol’ iliyomo ndani ya kitakasa mikono ndicho kiambata muhimu kinachotumika kuua vidudu.

Unatakiwa kuangalia uuaji wa wadudu pamoja na muda ambao wadudu hao watakufa, tunaweka wadudu hao kitaalamu kwa muda maalum, tukikuta wamekufa, tunajua kitakasa mikono hicho kinaweza kufanya kazi,” anasema.

Anasema Kiwango cha pombe kisipofika asilimia 60 inakuwa haina uwezo wa kuua vidudu, hivyo tunapima kuhakikisha kimefikia, kabla hata ya kuruhusu bidhaa kuingia sokoni, pia kuna vipimo vingine vya Micro-Biology ambavyo tunaita Challenge Test.

Naye Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa, Sophia Mziray, anasema Mamlaka hiyo imedhamiria kwa dhati kuifanya maabara hiyo ya Kanda kuwa bora na maalumu kwa uchunguzi vipukusi.

“Hivi sasa maabara hiyo ya kanda ya ziwa ndiyo pekee kwa Nchi wanachama wa Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye uwezo wa kupima vipukusi na kutoa majibu yasiyo na shaka. Anaongeza Sophia Mziray.

“Na kwa kuwa ni maabara pekee katika Kanda ya Ziwa, hivyo tunaendelea pia kuchunguza dawa kutoka kanda nyingine, kutoa elimu kwa umma, na kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa bora, salama na zenye ufanisi.

“Mpango huu tunaotarajia utakamilika ndani ya miaka mitatu kuanza sasa, maabara hii ipo kwenye taratibu kuwa kubwa, ya kisasa, bora na bobezi katika uchunguzi wa vipukusi katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na hata Bara zima la Afrika,” amesema.

Anaongeza kuwa  Maabara hii ina mifumo ambayo imethibitishwa. Mamlaka inaandaa nyaraka, upembuzi yakinifu kujiridhisha kama rasilimali zinatosheleza ili kutimiza nia ya kuwa na maabara bora zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post