WADAU WA TIBA ASILI WATAKIWA KUJIPANGA KUUSHIKA UCHUMI WA MAUZO YA DAWA ASILI NA MIMEA DAWA KIMATAIFA


Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame akitoa hotuba ya uzinduzi wa jukwaa hili. 
Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzindua rasmi jukwaa. 
Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko akitia neno kwa wagana hao wa tiba asili na wadau wengine wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo. 
Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki akieleza kwa kifupia majukumua na malengo ya mradi huo wa GRILI na yale ambayo yamefanyika toka mradi uanzishwe. 
Wadau wa tiba sili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wakifuatilia hotuba na maneno ya uzunduzi wa Jukwaa lao kutoka kwa viongozi.

*****************************

NA: Calvin Gwabara - Morogoro.

Wataalamu wa chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa tiba asili na taasisi zingine katika kufanya tafiti za dawa ambazo zitasaidia dunia katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID 19 na magonjwa mengine hatari kwa afya ya binadamu,Wanyama na hata mimea kwani takwimu nchini Tanzania zinaonyesha tiba asili inatoa mchango wa zaidi ya asilimia 45 katika unga wa matibabu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame kwa niaba ya Katibu mkuu wa wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ubunifu la wadau wa tiba asili Tanzania uliofanyika SUA mkoani Morogoro.

Dkt.Mhame amesema kuwa Tiba asili inayo nafasi kubwa katika kukabiliana na magonjwa hayo ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuzuaia na kutibu na ndio maana kuna sheria ya tiba asili na tiba mbadala Na.23 2002.

“Upatikanaji a tiba asili na tiba mbadala inayotokana na mimea dawa itasaidia sana kufikia wananchi wengi hasa wanaoishi vijijini hivyo nimefurahishwa na malengo ya jukwaa hili kwani yanaendana na malengo ya serikali kupitia wizara yetu hii ya afya ya kuhakikisha tunaboresha afya za wananchi wetu kupitia za kisasa na tiba asili” Alisema Dkt. Mhame.

Amefafanua kuwa biashara ya tiba asili duniani inakuwa kwa kasi sana kwani kwa takwimu za shirika la fya duniani WHO zinasema mwaka 2000 mauzo yake yalikuwa dola za kimarekani bilioni 20,mwaka 2012 ilipanda na kufikia dola za kimarekani bilioni 60,Mwaka 2018 ikafikia dola bilioni 80 na sasa inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 mauzo ya tiba asili yatafikia dola za kimarekani trilioni 3.

“Kwahiyo niwaombe sana ndugu zangu watafiti wa SUA na waganga wa tiba asili nchini kushirikiana ili kusaidia kujipanga vizuri ili Tanzania nayo inufaike kama China na nchi zingine duniani kwenye mauzo ya dawa za tiba asili wakati yakielekea kufikia Trilioni 3” Alisistiza Dkt. Mhame.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi huyo kuzindua jukwaa hilo Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la jukwaa hilo ni kuibua ubunifu nna kutatua changamoto zilizoko kwenye mnyaroro wa thamani wa biashara ya bidhaa za miti mimea dawa Tanzania ili iweze kuwa endelevu na kutoa mchango mkubwa kwenye kipato cha Wananchi na Tanzania kwa ujumla.

“Malengo ya Chuo chetu pia yanahusisha uendelezaji wa maarifa na ujuzi,bunifu,busaraza kitaalamu na uelewa kupitia mafunzo,matokeo ya tafiti,huduma za ugani na ushauri wa kitaalamu na katika uzalishajiu hivyo tunaamini kuwa uratibu wetu wa kuanzisha jukwaa hili uko kwenye mojawapo ya majukumu yetu na malengo ya uanzishwaji wa chuo chetu” Alifafanua Prof. Mhaurwa.

Aliongeza kuwa SUA kupitia watafiti wake kwenye mradi huu wamefanya tafiti nyingi ambazo zimeonesha kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya tiba asili na mimea dawa hasa ubunifu mchache unaoibuliwa kwenye biashara hii,SUA imeona ni vyema kutumia uzoefu wake wa ndani kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu uanzishwaji wa jukwaa hili.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewataka waganga hao wa tiba asili kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kupima viambata mbalimbali vinavyopatikana kwenye dawa zao ili kusaidia kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wateja wao endapo dawa itakuwa na viambata ambavyo sio salama.

“Kazi ya ofisi yangu sio kuzuaia nyinyi kupata usajili wa dawa zenu bali tunataka kuona kila dawa mnayoitoa kwa wagonjwa iwe na viambata sahihi ili iweze kutibu vizuri na isilete madhara kwa wateja wenu lakini pia upimaji wetu ndio wa mwisho ili muweze kupata usajili wadawa tukiweka sahihi yetu kuwa dawa iko salama hakuna wa kupinga hivyo msiogope tushirikiane” Alisema Dkt. Mafumiko.

Mkemia mkuu huyo wa serikali alisema kuwa malengo ya waganga wa tiba asili na malengo ya ofisi yake ni moja tuu kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa dawa hizo na ofisi yake inavyo vifaa na wataalamu wa kutosha kubaini kila kilicho kwenye dawa hivyo wale wachache wanaofanya udanganyifu waache maana watabainika.

Pia Dkt. Mafumiko ameipongeza SUA na watalaamu wake kwa jitihada kuwa wanazozichukua katika kuwasaidia waganga hao wa tiba asili kuweza kuboresha huduma ya tiba wanayoitoa kwa Jamii ili iweze kuwa bora na yenye viwango vinavyohitajika.

Mkemia mkuu huyo wa Serikali iliahidi kushirkiana na SUA kwenye mpango huo ili uweze kuleta tija inayokusudiwa kwa jamii na taifa kupitia wataalamu wa ofisi yake muda wowote watakapohitajika.

Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki alisema kuwa toka mradi huo uanze mwaka 2018 umekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau wa tiba asili Tanzania nab ado unaendelea kushirikiana nao kuhakikisha biashara ya tiba asili na mimea dawa inachangia uchumi wa wadau hao na taifa.

“ Wakati tunaanza mradi huu mwaka 2018 waganga wengi hapa wa tiba asili walikuwa wanauza dawa zao kwenye mkifuko ya Rambo,magunia na vifungashio vingine visovyo na ubora lakini tunafurahi leo wakati tunazindua jukwaa hili tunaona wote wameweka dawa kwenye vifungashio bora na vye viwango vinavyokubalika kitaalamu.”Alisema Alifafanua Dkt. Mabiki.

Aliongeza “Lengo letu ni kutaka kuona biashara ya mimea dawa na uuzaji wa dawa za asili haufanyiki tuu hapa nchini bali wataalamu hawa wa tiba asili waweze kufungasha vizuri na kuuza hadi nje ya nchi na kupata mapato wao wenyewe lakini pia na taifa kama ambavyo ilivyo kwa nchi nyingine duniani kama China na India”.

Dkt. Mabiki alisema ili hilo lifanikiwe pia lazima kuwe na uendelevu wa upatikanaji wa mimea dawa hiyo ili pale inapohitajika kwa wingi iweze kupatikana na ndio maana mradi unawafundisha namna ya kuanzisha mashamba ya mimea dawa ili waweze kulima na kuipata kwa wingi na kirahisi pale inapohitajika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments