MWENYEKITI HALMASHAURI TARIME NA MKEWE WATEMBELEA WAFUNGWA MAHABUSU GEREZA LA TARIME … WATOA MSAADA WA NGUO,VYAKULA NA FEDHAMwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa kata ya Nyakonga Simion Samwel akimkabidhi kaimu mkuu wa gereza la wilaya ya Tarime aliyevaa (kofia) Francis Makelemo gunia za mchele,sabuni,mafuta kwa ajili ya wafungwa na mahabusu.
Ester Simion mke wa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel akitoa kanga kwa ajili ya wafungwa gereza la Tarime

Na Dinna Maningo, Tarime
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa kata ya Nyakonga Simion Samwel  akiwa ameambatana na mke wa mke Ester Simion wamewatembelea wafungwa na mahabusu katika gereza la wilaya ya Tarime na kutumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kutoa msaada wa huduma za kiroho na kimwili.

Akiwa ameambatana pia na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka na Katibu Mwenezi wa CCM wilaya hiyo Marema Sollo leo Jumapili Januari 24,2021 , Simion amemkabidhi Kaimu Mkuu wa gereza wilaya ya Tarime, Francis Makelemo mchele kilo 480, sabuni za miche maboksi 10, sabuni za unga mifuko 22, mafuta ya kula ndoo 5 na kanga pea 40, pesa taslimu sh. 620,000/= kwa ajili ya watu wanaoletewa chakula nje vyote vikighalimu  jumla ya sh.Milioni tatu.

"Mimi ni muumini wa kanisa la Wasabato la Turwa na huwa tunatoa msaada kwa wahitaji,kutembelea wagonjwa,wafungwa na wengine wenye uhitaji,mimi na mke wangu tumewiwa kutoa fedha zetu za mfukoni ili wafungwa na mahabusu wapate huduma ya kimwili. Nawaomba na wengine wasaidie", alisema Simion.

Ester Simion alisema kuwa kwa kuwa yeye ni mama ameguswa kuwasaidia wanawake walioko gerezani kwa kuwanunulia kanga pea 40 zenye thamani ya sh.320,000/= na kuwaasa akina mama kusaidia wahitaji kwa chochote walicho nacho hata kama ni kidogo.

Mchungaji wa kanisa la Waandventista wasabato Turwa Joseph Iteremi alisema katika maandiko ya biblia Mathayo 25 inazungumzia kuwajali na kuwatembelea wahitaji na kanisa hilo pamoja na waumini wake huwatembelea wahitaji na kuwasaidia kwakuwa ni sehemu ya utume.

"Nimshukuru Mwenyekiti wa halmashauri kwa moyo wake wa kuwasaidia  wahitaji na kuwakumbuka wafungwa gerezani ,na niwashukuru askari wa gereza wamekuwa wakiwahudumia vizuri wafungwa lakini kutoa nafasi ya watu kuwatembelea na kuwaona wafungwa na mahabusu tuendelee na moyo huohuo wa kusaidia", alisema Iteremi.

Katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka alisema kuwa kufungwa ni sehemu ya adhabu kwa ajili ya kujirekebisha hivyo wafungwa wana haki ya kupata huduma sawa na wengine huku akimpongeza mwenyekiti huyo kwa msaada alioutoa na kusema kuwa Chama Cha Mapinduzi kinampongeza kwa kuwa matendo mazuri ukifanya chama kizidi kuaminiwa.

Kaimu mkuu wa Gereza wilaya ya Tarime Francis Makelemo alisema kuwa gereza hilo lina jumla ya wafungwa na mahabusu wapatao 532 kati ya hao wafungwa ni 117 na mahabusu ni 415,alimshukuru mwenyekiti Simion kwa moyo wake wa kuwajali mahabusu na wafungwa na msaada alioitoa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa kata ya Nyakonga Simion Samwel akimkabidhi kaimu mkuu wa gereza la wilaya ya Tarime aliyevaa (kofia) Francis Makelemo gunia za mchele,sabuni,mafuta kwa ajili ya wafungwa na mahabusu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post