WAZIRI MWAMBE ATOA SIKU 7 KILA TAASISI KUPELEKA MIPANGO MIKAKATI YAO OFISINI KWAKE

Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Geoffrey Mwambe akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo alipokutana nao Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.

Naibu Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Exaud Kigahe akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo( hawapo pichani) wakati wa kikao cha Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, alipokutana nao Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.

Baadhi ya Watumishi mbalimbali wa Wizara ya Viwanda na biashara wakimsikiliza Waziri wa Viwanda na biashara Mhe. Geoffrey Mwambe (hayupo pichani) walipokutana na Waziri wa Wizara hiyo Jijini Dodoma kuweka mikakati ya pamoja namna ya kuendeleza wizara hiyo na kuleta matokeo chanya.

Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Geoffrey Mwambe amewaagiza Wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara hiyo kutengeneza taarifa ya mawasilisho ya majukumu watakayoyafanya kwa mwaka huu wa fedha.

Pia ametoa siku saba (7) kwa taasisi hizo kupeleka kwake ukomo wa bajeti na mikakati ya tofauti waliojiwekea kwaajili ya kuendeleza na kuleta mabadiliko katika taasisi hizo.

Waziri Mwambe ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokutana na wakuu wa taasisi zilizochini ya Wizara yake, Wakuu wa idara na wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo amesema kila taasisi ihakikishe imeweka mikakati mipya ya kuleta mabadiliko katika sekta ya Viwanda na biashara.

"Ndani ya siku saba (7) kila taasisi itengeneze taarifa na iwasilishwe kwangu juu ya mikakati mikubwa ya kufanyakazi na kuleta mabadiliko makubwa, kama wewe BRELA tuletee mikakati yako umepanga kufanya nini" amesema Mhe Mwambe.

Ametaka kila kitengo katika Wizara hiyo kujitafakari wanafanyaje kazi na wamejipangaje katika kuleta mabadiliko makubwa katika sekta yao ili kuimarisha sekta ya Viwanda na biashara iweze kulinufaisha taifa.

Aidha ametaka watumishi hao kuwa wabunifu katika nafasi zao za kazi na kutengeneza kitu cha tofauti katika utumishi wao utakaoleta mabadiliko chanya katika sekta ya Viwanda na biashara hapa nchini.

Pia amezitaka taasisi hizo kutengeneza mifumo mipya ya utafutaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini zipate masoko ya ndani na nje ya nchi.

"Tuanze kutafuta masoko ya bidhaa zetu kuna wajasiliamali wanatengeneza bidhaa lakini hawana masoko hawa tunawakatisha tamaa, lakini akizalisha bidhaa na akapata soko inampa nguvu kuendelea kuzalisha zaidi"

"Tuwe wabunifu kuna kiwanda nilikitembelea kinazalisha maziwa lakini vifungashio wanafuata Kenya, namuuliza anasema hapa nchini hukuna, nikapita kiwanda kingine wanatengeneza vifungashio vilevile nae anasema hana soko hapa tunafanya uzembe hatuwauganishi hawa wazalishaji" amesema Mhe Mwambe.

Amesema kwa Sasa kuna masoko makubwa ya nje ya nchi ya bidhaa ambapo zinapatikana hapa nchini tena kwa wingi ni wajibu wa taasisi zinazohusika kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa hizo na kutafuta masoko hayo.

Ameonya baadhi ya watumishi wa taasisi na Wizara kwa kuwa vikwazo kwa kishelewesha majibu ya maombi ya wafanyabiashara wanapotaka huduma katika ofisi hizo kwa kuchelewesha kwa makusudi.

"Unakuta mtumishi wa TBS anashirikiana na mshindani wa muomba vibali huyu kila akileta maombi ya kuthibitishwa anaambiwa hajakidhi viwango kumbe wewe unazunguka upande wa pili unachukua fedha" amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na biashara Mheshimiwa Exaud Kigahe, amewataka watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuleta matokeo chanya katika Wizara hiyo.

"Nataka mshirikiane muwe wamoja mtekeleze mahukumu yenu kwa uadilifu na kuwa kiunganishi imara kati ya wafanyabiashara, wakulima na masoko ya bidhaa zao" amesema Mhe. Kigahe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post