Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Dkt. MAGILIGIMBA ASHIRIKI KIKAO CHA BODI YA IAWP NCHINI MAREKANI

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Dkt. Debora Magiligimba ameshiriki kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Polisi Wanawake Duniani (International Association of Women Police IAWP) kinachofanyika katika jiji la Flagstaff Jimbo la Arizona nchini Marekani.

Kikao hicho cha Bodi kinafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 11 Machi 2026 hadi 12 Machi 2026, kikihusisha viongozi waandamizi wa IAWP kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Shirikisho la Polisi Wanawake Duniani pamoja na namna bora ya kuendelea kuimarisha uwepo na mchango wa wanawake wote wanaotekeleza majukumu yao katika vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi duniani katika ukanda wa Region 21 ambao anausimamia.

Miongoni mwa ajenda kuu zinazojadiliwa katika kikao hicho ni maandalizi ya Mkutano na Mafunzo ya Kimataifa ya Mwaka 2026 (IAWP Annual Training Conference) utakaofanyika Bali nchini Indonesia. Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha maafisa wa Polisi wanawake kutoka nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa kitaaluma pamoja na kujadili mikakati ya kuimarisha uongozi wa wanawake katika sekta ya usalama.

Aidha, mkakati wa IAWP katika kuimarisha nafasi ya wanawake ndani ya vyombo vya polisi umejengwa katika nguzo nne muhimu ambazo ni Kuendeleza uongozi kwa wanawake katika Jeshi la Polisi, Kujenga uwezo kupitia elimu na mafunzo mbalimbali ya kitaaluma, Kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kati ya mashirika na taasisi za usalama, Kushughulikia changamoto za kuajiri na kuhifadhi rasilimali watu katika vyombo vya polisi.

IAWP inaendelea kukuza uongozi wa wanawake katika jeshi la polisi duniani na imejitolea kuhakikisha sauti zao zinasikika katika kila ngazi ya kufanya maamuzi, Kupitia urithi wake uliojengwa kwa muda mrefu pamoja na mtandao mpana wa kimataifa, shirikisho hilo lina nafasi kubwa ya kuongoza katika kushughulikia na kushinda changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanawake katika taaluma ya polisi, na hivyo kuwawezesha kuchangia kikamilifu katika kujenga dunia salama zaidi.

Dhamira na maono ya shirikisho hilo la askari wa kike duniani (IAWP) yanaongozwa na Katiba na Kanuni za shirika (Bylaws) ambazo zinaelekeza utekelezaji wa majukumu na malengo ya shirikisho hilo kimataifa.

Kupitia ushiriki wake katika kikao hicho, Dkt. Magiligimba anaendelea kuiwakilisha Tanzania na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kimataifa, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji pamoja na kutafuta fursa za mafunzo na maendeleo kwa maafisa wa Polisi wanawake nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com