WITO umetolewa kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kuwapa uangalizi wa karibu vijana wanaomaliza kidato cha nne ili kuwanusuru kutumbukia kwenye majanga yanayoweza kuhatarisha mustakabali mzuri wa ndoto zao.
Akihutubia sherehe za mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Utaho, iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, Kaimu Afisa Vijana mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Dkt Rehema Nchimbi, alisema ni jukumu la mzazi kupokea kijiti kile kile cha mwendelezo wa maadili mema kutoka kwa walimu wao, pindi vijana wawapo majumbani.
"Wazazi msiwe mbali na vijana hawa, tushirikiane kuhakikisha kile walichojifunza shuleni hata wakiwa nyumbani wanaendelea kukiishi katika misingi ya uzalendo," alisema Ndahani.
Alisema mustakabali chanya wa maendeleo ya Tanzania katika muktadha wa ustawi wa kiuchumi, amani na usalama wa nchi upo mikononi mwa vijana hao, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwatupia jicho la karibu katika kipindi hiki wanapoandaliwa kimasomo.
Pamoja na mambo mengine, aliwasisitiza wazazi katika kipindi hiki kuwa makini dhidi ya genge baya la wasafirishaji haramu wa binadamu wanaopita-pita kuwarubuni vijana, hususani watoto wa kike mkoani hapa kwa kigezo cha kwenda kuwatafutia ajira zenye maslahi makubwa jambo ambalo sio la kweli.
“Katika hili wazazi tuchukue tahadhari kubwa…hali siyo ya kuridhisha kutokana na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa maslahi ya waliowasafirisha” alisema Ndahani.
Aidha, akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa Nchimbi kwa vijana hao, Ndahani alisema Rais John Magufuli anaipenda sana Singida, na ndio maana hivi karibuni amekabidhi shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa sekondari hiyo ya Utaho.
Alisema juhudi za kukabiliana na changamoto nyingine zilizopo, ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu na maabara vitaendelea kuzingatiwa na kushughulikiwa ipasavyo, ili kuhakikisha Utaho naendelea kuwa kitovu cha elimu ndani ya mkoa.
Awali, Ndahani akiwa kwenye eneo hilo la Utaho, alipata fursa ya kutembelea na kukagua mradi wa aina yake wa shamba bora la zao la embe linalomilikiwa na mwekezaji mzawa, Aqlan Gharib maarufu "Turu Best" na aliwasihi wana-singida kwenda kujifunza teknolojia za kilimo hicho chenye tija kwa ustawi wa lishe na ongezeko la kipato.