ACT WAZALENDO YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA ASKOFU WA JIMBO KATOLIKI TANGA ANTONY BANZI


Askofu wa Jimbo la Katoliki Tanga, Anthony Banzi enzi za uhai wake.
***
Chama cha ACT-Wazalendo, kimetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo la Katoliki Tanga, Anthony Banzi. 

Askofu Banzi amefariki dunia leo tarehe 20 Desemba 2020, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) alipokiwa amelazwa kwa ajili ya matibabu. Taarifa za kifo cha Askofu Banzi zimetolewa na Padre Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza Katoliki la Maaskofu Tanzania (TEC) mapema leo asubuhi na kueleza kuwa tarehe ya mazishi itatolewa baadaye.

“Baraza la Maaskofu Tanzania linasikitika kutangaza kifo cha Baba Askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Katoliki Tanga, amefariki leo tarehe 20 Desemba 2020 na tarehe ya mazishi tutajulishwa baadaye,” ilieleza taarifa hiyo.

Kufuatia kifo hicho, Chama cha ACT-Wazalendo kimetuma salamu zake za rambirambi kupitia kwa Janeth Rithe, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa chama hicho na kimeeleza kusikitishwa na taarifa hizo za kifo ambapo amesema, chama hicho kinatoa pole kwa familia ya Askofu, ndugu na jamaa na kuwataka kuwa na subira katika wakati huu wa msiba.

“Chama cha ACT-Wazalendo kimehuzunishwa na taarifa ya kifo cha Baba Askofu Anthony Banzi wa Jimbo la Katoliki la Tanga kilichotokea leo tarehe 20 Desemba 2020 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,

“Katika uhai wake, Baba Askofu Banzi amelitumikia Taifa kiroho kwa upendo mkubwa, Chama cha ACT-Wazaleno kinatuma salamu za pole kwa kanisa la Katoliki Jimbo la Tanga, kwa wakatoliki wote na watu wote walioguswa kwa namna moja ama nyingine, Mungu awape faraha katika kipindi hichi kigumu,” imeeleza taarifa hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments