VIZIWI WAWEZESHWA KUFANYA KAZI KWA USALAMA

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, akifungua mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa watu wenye changamoto ya kusikia (Viziwi) mkoani Mbeya. Kulia kwake ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda na kushoto ni Katibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA), Kelvin Nyema.Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akifunga mafunzo ya Usalama na Afya kwa watu wenye changamoto ya kutosikia wa Mkoa wa Mbeya. Alioambatana nao ni Kaimu Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Faston Uswege (Wa kwanza kushoto) na viongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania.Mwezeshaji kutoka OSHA, Simon Lwaho, akizielezea picha kuhusu usalama wa umeme zilizochapishwa katika bango wakati wa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi yalitolewa kwa viziwi mkoani Mbeya.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa watu wenye changamoto ya kutosikia wa Mkoa wa Mbeya wakifuatilia moja ya mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wawezeshaji kutoka OSHA. Mwezeshaji kutoka OSHA, Renatus Qaqal, akionyesha matumizi sahihi ya kofia ngumu katika sehemu ya kazi alipokuwa akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi yalitolewa kwa viziwi mkoani Mbeya.


Na Mwandishi Wetu

Kufuatia mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika shughuli za uzalishaji nchini, serikali imesema kuna umuhimu wa kuwawezesha kupitia mafunzo ya usalama na afya kazini pamoja na kuwapa mitaji ili wawaze kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kukuza uelewa wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Mkoa wa Mbeya.

Mafunzo hayo ya siku moja yalijikita katika kuainisha na kushauri mbinu mahsusi za kudhibiti vihatarishi vya usalama na afya ambavyo huambatana na shughuli mbali mbali za uzalishaji ikiwemo ujenzi, kilimo, useremala, kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo pamoja na kazi za maofisini.

Miongoni mwa vihatarishi vilivyoainishwa na watalaam wa OSHA katika mafunzo hayo ni pamoja na; vumbi, kelele, kemikali, umeme, mitambo na zana mbali mbali za kazi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo, Mkuu wa Wilaya amesema: “Pamoja na serikali kutenga fungu maalum la fedha kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi mbali mbali katika jamii ambapo asilimia mbili (2%) ya fedha hizo ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kama serikali tunaona kuna umuhimu wa kutoa mafunzo ya Usalama na Afya kwa makundi lengwa ili waweze kuepuka madhara yanaweza kusababishwa na kutozingatia kanuni za usalama na afya kazini.”

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliipongeza Taasisi ya OSHA kwa kutekeleza ipasavyo wajibu wake ikiwemo kufanya kaguzi za Usalama na Afya katika sehemu nyingi za kazi pamoja na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala ya Afya na Usalama kazini na kuitaka kuongeza jitihada zaidi ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa makundi mbali mbali ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu katika mikoa mbali mbali na kusisitiza kwamba mafunzo hayo ni endelevu.

“Kama Taasisi yenye dhamana ya Usalama na Afya kwa mfanyakazi, tumeona kuna umuhimu wa kuyafikia makundi haya ya watu wenye ulemavu kwakuwa tunatambua kwamba ulemavu ni hali tu na haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu kushiriki katika shughuli kiuzalishaji.

"Tumeshayafikia makundi mbali mbali ya watu wenye ulemavu katika mikoa kadhaa ikiwemo Kagera, Dar es Salaam, Pwani na sasa Mbeya na tutaendelea kutoa mafunzo haya katika mikoa mingine,” alieleza Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi.

Alisema baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Renatha Exsavery ambaye ni mwanafunzi wa ufundi katika Chuo cha VETA Mbeya na Queen Majembe wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo waliyoyapata ambapo wamesema mafunzo hayo yatawawezesha kujilinda dhidi ya vihatarishi mbali mbali vilivyopo katika sehemu zao za kazi.

“Mafunzo haya tuliyoyapata leo tumeyaona yanafaida nyingi kwani yatatusaidia kulinda afya zetu na kupitia mafunzo haya tutakuwa waangalifu zaidi katika kazi mbali mbali ambazo ni hatarishi hususan kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga muhimu,” alisema Renatha Exsavery, Mshiriki wa Mafunzo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments