MWAKILISHI MTEULE ACT-WAZALENDO AFARIKI DUNIA

 


MWAKILISHI Mteule wa Pandani kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Abubakar Khamis Bakar (69) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano tarehe 11 Novemba 2020, akiwa nyumbani kwake Mbweni visiwani Unguja, Zanzibar. 

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu wa Idara ya Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani.


Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake Mbweni, Unguja, atasaliwa alasiri katika Msikiti wa Qabus, uliopo Mazizini na kuzikwa Kianga, Wilaya ya Magharibi 'A' alasiri ya leo.

Abubakar Khamis, pia ni mjumbe wa kamati kuu ya chama na mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama cha ACT Wazalendo.

Abubakar Khamis Bakar, aliwahi kuwa mwandishi wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Mjumbe wa zamani wa Baraza Kuu la CUF.

Mbali na hayo aliwahi kuwa ni mjumbe wa zamani wa kamati ya kutafuta mwafaka Zanzibar, mjumbe pia wa zamani wa kamati iliyofanikisha kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Pia aliwahi kushika nyadhifa ya kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa 2010 - 2015.

Na mpaka mauti yanamfika alikuwa ni mwakilishi mteule wa kuchaguliwa na wananchi katika jimbo la Pandani, Pemba, kupitia Chama Cha ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanya Oktoba 27 na 28 mwaka huu.

Abubakar Khamis Bakar, amezaliwa Novemba 02, 1951 na amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo Jumatano, Novemba 11, 2020.
 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments