GEMMA ASHAURI WANAUME WAWE NA NIDHAMU KWENYE NDOA ZAO ...."ACHENI KUBAKA WAKE ZENU"

 
Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Bi. Gemma Akilimali akielezea madhara yanatokana na vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa na kusisitiza umuhimu wa wanandoa kushirikishana katika masuala yanayohusu familia.
Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Bi. Gemma Akilimali akielezea madhara yanatokana na vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa.
 *** 

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Imeelezwa kuwa ukosefu wa nidhamu katika tendo la ndoa unachangia kuwepo vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa hali inayosababisha wanawake kuathirika kisaikolojia pindi wanapopata ujauzito bila kutarajia kwa kubakwa na waume zao. 

Hayo yamesemwa leo na Mwanaharakati wa masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu, Bi. Gemma Akilimali wakati akitoa mafunzo juu  ya Bajeti kwa mtazamo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa UNFPA na KOICA.

Katika kutoa mada hiyo kumejitokeza mjadala mzito wa familia kuelemewa na watoto wengi na lawama kwenda kwa wanawake kwamba hawakubali kuzaa kwa mpango hivyo kujaza familia hali inayosababisha wazazi washindwe kuzihudumia na wakati mwingine kutelekezana. 

Gemma alisema kukosekana kwa nidhamu ya mahusiano baina ya wanandoa ikiwemo kushirikishana, kunachangia vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa matokeo yake wanawake wanapata ujauzito bila kutarajia hivyo kuathiri maisha yao.  

“Ubakaji ndani ya ndoa unasababisha mama kupata ujauzito bila kutarajia matokeo yake unamfanya mwanamke ashindwe kutekeleza majukumu aliyokuwa amepanga kuyatekeleza kwa kuanza kulea mimba hali ambayo pia inamuathiri kisaikolojia”,alisema Gemma. 

“Uhusiano wako na mke wako na upendo wenu ni rasilimali ya familia,ukizaa bila mipango unatawanya rasilimali zako matokeo yake utajikuta haupigi hatua za kimaendeleo. Kama kunaongezeko la familia pia mgawanyo wa rasilimali unaongezeka”,alieleza Gemma. 

Pia aligusia kuhusu suala la ubakaji ndani ya ndoa na kueleza kuwa hii wakati mwingine inasababisha watoto wazaliwe bila mipango na hivyo kuongeza mzigo wa kuwahudumia katika maisha yao. 

“Mwanaume usimlaumu mkeo kuwa na watoto wengi wakati ulimbaka mkazaa bila mipango. Mbaya zaidi familia inapokuwa kubwa wengine mnashindwa kuhudumia watoto kutokana na kwamba umeshindwa kupangilia mambo yako vizuri”,alisema.  

“Lazima kuwe na mipango katika familia. Baba na mama washauriane kuhusu idadi ya watoto ili iendane na uwezo wao wa kuihudumia . Hii inaendana na kupanga bajeti kwa mtazamo wa kijinsia ili familia iweze kutekeleza majukumu ya maendeleo ya kifamilia na kijamii kwa upendo na furaha na hivyo kuchochea maendeleo”,alifafanua Gemma. 

Aidha alishauri ili kupiga hatua kimaendeleo ni vyema kutazama kila jambo kwa jicho la mrengo wa kijinsia na kupunguza kununua au kutoa fedha kwa kila kitu hata visivyo katika mipango yako akisisitiza kuwa kila mtu ni tajiri lakini tatizo kuna matumizi holela ya fedha na rasilimali. 

 

“Mabadiliko yaanzia katika familia yako, Ukitazama kila kitu kwa mrengo wa kijinsia hakika utapata mabadiliko makubwa kimaendeleo. Angalia kipi ununue,kipi ufanye. Jiulize hiyo michango unayochangia ina misingi gani kwako, mfano kuna mwingine hata kama hana pesa yupo tayari kukopa ili achangie harusi au Kitchen Party badala ya kupeleka mtoto shule”,ameongeza Gemma.  

Katika hatua nyingine ameeleza kusikitikishwa na tabia ya baadhi ya wazazi kukwepa kulea watoto wao na matokeo yake wanapeleka watoto kwa bibi zao bila hata ya kupeleka rasilimali za kusaidia watoto hao hivyo kuwaongezea mzigo wa malezi japokuwa umri wao umeenda na hawawezi kuzalisha mali kutokana na uzee hivyo kusababisha umaskini kuendelea katika familia.


Soma pia : 

TGNP YATOA MAFUNZO YA JINSIA KWA VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA,WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI MSALALA




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments