WAZAZI MSALALA WAONYWA KUOGESHA WANAFUNZI DAWA ZA MVUTO WA MAPENZI 'SAMBA'

Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Msalala Neema Katengesya 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga wametakiwa kuachana na tabia ya kuwatengenezea 'kuwaogesha' dawa za mvuto wa mapenzi ‘Samba’ wanafunzi wa kike kwani inachangia kuwepo kwa mimba na ndoa za utotoni hali inasababisha ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii. 

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 11,2020 na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Msalala Neema Katengesya wakati wa mafunzo ya kubadilisha mtazamo wa kifikra kuhusu masuala ya jinsia na elimu juu ya mipango na bajeti zenye mrengo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga. 

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa UNFPA na KOICA, Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Msalala, Neema Katengesya aliitaka jamii kuachana na mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike ikiwemo kupeleka kwa waganga wa jadi watoto wa kike wakiwemo wanafunzi kuoshwa dawa ili wawavutie wanaume waolewe. 

“Wazazi na walezi acheni kuwatengenezea dawa za mvuto wa mapenzi wanafunzi. Haiwezekani mtoto atembee kama bidhaa mtaani kuvutia wanaume kwani tunaharibu watoto wetu. Watoto wanashindwa kusoma wakiwaza kuolewa tu na wengine kujikuta wakipewa ujauzito na kukatisha masomo yao”,amesema Katengesya. 

“Kila mtu anazaliwa na nyota yake,Mganga wa jadi hana cha kukupatia nyota ndugu zangu. Tusiwachafue watoto wetu,tuwaacheni wasome ili waje kuwa watalaamu wetu wa kesho”,ameongeza Katengesya. 

Kwa upande wake, Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gemma Akilimali ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya jinsia na haki za binadamu amesema suala la watoto kuogeshwa dawa ili wapendwe na wanaume linatakiwa kupigiwa kelele na kila mpenda maendeleo. 

“Sisi kama TGNP tungependa washiriki wa mafunzo haya wakiwemo maafisa watendaji wa vijiji na kata pamoja na Wana Vituo vya Taarifa na Maarifa wabadilike kimtazamo ili mkatumie mafunzo haya tuliyowapa kutoa elimu kwa jamii iachane na mila na desturi zinazokandamiza wanawake na watoto ili jamii iwe na furaha”,amesema Gemma. 

Mwanaharakati huyo wa masuala ya jinsia na haki za wanawake amesisitiza pia kuhusu umuhimu wa kuwapatia elimu watoto wa kike na wa kiume ili kuwa na usawa katika jamii na kwamba mabadiliko hayahitaji malumbano bali yafanyike kwa upendo ili kuepuka kundi moja kunyimwa haki. 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Dotto Shija, Loyce Kabanza, Maria Ntowe na Godrey Justine wamezitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili jamii ni mimba na ndoa za utotoni, mfumo dume,wanawake kutoshirikishwa katika maamuzi kuanzia ngazi ya familia na kutopewa haki ya kumiliki rasilimali. 

Wamesema ili kutatua changamoto ni vyema elimu itolewe kwa jamii kuhusu ushirikishwaji wa wanawake na madhara ya mimba na ndoa za utotoni lakini pia kuhimiza watoto waliofikia umri wa kwenda shule wapelekwe shule na kuhamasisha wanawake kujiamini ili kupigania haki zao. 
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Msalala Neema Katengesya akizungumza wakati wa mafunzo ya kubadilisha mtazamo wa kifikra kuhusu masuala ya jinsia na elimu juu ya mipango na bajeti zenye mrengo wa kijinsia kwa Wanajamii na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga.  leo Jumatano Novemba 11,2020 katika ukumbi wa Mabingwa Bugarama halmashauri ya wilaya ya Msalala. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Msalala Neema Katengesya akiwahamasisha maafisa watendaji wa vijiji na kata na vituo vya taarifa na maarifa kutoa elimu kwa jamii kuachana na mila na desturi zisizofaa ikiwemo kuogesha dawa za mvuto watoto wa kike ili waolewe.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gemma Akilimali ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya jinsia na haki za binadamu akielezea madhara ya watoto kuogeshwa dawa ili wapendwe na wanaume na kusisitiza lipigiwe kelele na kila mpenda maendeleo. 
Mwezeshaji wa mafunzo, Magdalena George akizungumza wakati wa mafunzo ya kubadilisha mtazamo wa kifikra kuhusu masuala ya jinsia na bajeti kwa mrengo wa kijinsia kwa Vituo vya Taarifa na Maarifa na Watendaji wa vijiji na kata za Shilela na Lunguya halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Magdalena George akitoa mwongozo wa majadiliano kuhusu changamoto zilizopo katika kata ya Shilela na Lunguya katika halmashauri ya wilaya ya Msalala. 
Washiriki wa mafunzo wakiendelea na kazi ya kikundi.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Mchungaji Godfrey Justine kutoka kanisa la EAGT kata ya Lunguya akieleza namna ya kutokomeza mila na desturi zisizofaa katika jamii.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Loyce Kabanza akichangia hoja namna ya kutokomeza mila na desturi kandamizi katika jamii.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments