BUNGE LAMTHIBITISHA KASSIM MAJALIWA KUWA WAZIRI MKUU WA TANZANIA..HII HAPA HISTORIA YAKE

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja leo tarehe 12 Novemba 2020 limemthibitisha Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha muhula wa pili wa serikali ya awamu ya tano.

Uteuzi wa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu umefanywa na Rais John Magufuli leo Alhamisi Novemba 12, 2020 na jina lake kuwasilishwa bungeni na mpambe wa Rais.

Baada ya kuwasilishwa, Spika Job Ndugai aliwatangazia wabunge kuhusu uteuzi huo, kisha wawakilishi hao wa wananchi kupiga kura ya kumthibitisha.

Katika ya kura 350 zilizopigwa, wabunge wote walipiga kura ya ndio kumuidhinisha Majaliwa kuwa mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali.

"Idadi ya kura zilizopigwa ni 350, hakuna kura yoyote iliyoharibika, kura ya hapana hakuna hata moja zote 350 zimemthibitisha Mhe.Kassim Majaliwa, kwa hiyo waheshimiwa wabunge Mhe, Kassim Majaliwa amethibitishwa na bunge hili kuwa Waziri Mkuu kamili", amesema Spika Ndugai.

Kassim Majaliwa atahudumu katika nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.


MAJALIWA KASSIM MAJALIWA NI NANI??
Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, ambaye anaendelea na wadhifa wa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa muhula wa pili, alizaliwa tarehe 22 Desemba mwaka 1960 yaani miaka 60 iliyopita.

Kitaaluma ni Mwalimu aliyepata elimu yake ya Ualimu katika chuo cha ualimu cha Mtwara mwaka 1991-1993, na baadae kujiendeleza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden.

Kutoka mwaka 1984 mpaka 2006 amehudumu katika nafasi mbalimbali kama mwalimu na kiongozi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT). 

Mwaka 2006 Majaliwa aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na kisha akajitosa kwenye siasa za ushindani mwaka 2010 alipogombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi.

Baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa serikali ya awamu ya nne.

Majaliwa ameidhinishwa kuwa Waziri Mkuu na Bunge baada ya jina lake kuwasilishwa bungeni na mpambe wa rais John Magufuli na kupigiwa kura ya ndiyo na wabunge wote 350 waliokuwepo ukumbini. Anatarajiwa kula kiapo hivi karibuni ili kuanza rasmi majukumu yake.

Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Magufuli uliokamilika mwezi uliopita.

 Endapo atadumu katika wadhifa huo kwa kipindi chote cha pili cha rais Magufuli atakuwa Waziri Mkuu wa pili kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo. Fredrick Sumaye, ndiye mtu pekee mpaka sasa aliyehudumu kwa miaka 10 mfululizo kama Waziri Mkuu wa Tanzania kutoka mwaka 1995 mpaka 2005 chini ya rais mstaafu hayati Benjamin Mkapa.

Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Magufuli uliokamilika mwezi uliopita.

Uteuzi wa Majaliwa hii leo haukushtua wengi kama alivyoteuliwa mara ya kwanza miaka mitano iliyopita. 

Wachambuzi wengi walitarajia Majaliwa kurejea katika nafasi yake, mosi kutokana na kauli ya rais Magufuli na pili kutokana na utendaji wake. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli alizungumza wakati wa tukio la kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, kwamba viongozi wa serikali hawatakiwi kuwa na hofu ya nafasi zao kwa sababu mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita yalitokana na ufanisi wao pia.

Ingawa alisema kutakuwa na mabadiliko makubwa katika baraza jipya la mawaziri, ni vigumu kutenganisha mafanikio ya utawala wa Awamu ya Tano na utendaji wa Waziri Mkuu. 

Katika mawaziri wote wa serikali ya Rais Magufuli, Majaliwa - kama kiranja wa mawaziri wengine, ndiye pekee ambaye nafasi yake inafungamanishwa moja kwa moja na Rais katika utendaji.

Majaliwa anatokea kusini mwa Tanzania eneo ambalo mtu wa mwisho kutoka ukanda huo kuwa waziri mkuu alikuwa Mzee Rashid Kawawa aliyekuwa Waziri Mkuu miaka ya mwanzoni ya uhuru. Yeye nimtu wa 11 kuwa Waziri Mkuu tangu Tanganyika ilipopata uhuru ambapo Waziri Mkuu wa kwanza alikuwa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa kila siku wa kazi na shughuli za Serikali, atakuwa na madaraka ya kuongoza shughuli za serikali Bungeni.

Atakuwa na madaraka ya kutekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo rais ataagiza yatekelezwe.

Pia Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa Mawaziri.

Anayo madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.

Waziri Mkuu huyu ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu, na pia amesomea ualimu wa mpira. Katika kipindi cha mwaka 2010-2015 alikuwa Kocha wa timu ya soka inayoundwa na wabunge.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments