Sifa ya Tanzania Duniani ni Umoja na Mshikamano – Rais Magufuli


Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha tunu ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili na kamwe wasikubali kuibomoa iwe kwa dini au kabila.

Akizungumza jana (Jumatatu, Oktoba 26, 2020) wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wakati  akizindua msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Rais Magufuli alisema kuwa  msikiti huo utumike kuwaweka pamoja kama ndugu, pia ukawe fundisho kwa wana Chamwino na watanzania katika kuwa wamoja na kutambua kuwa wana wajibu wa kumtanguliza Mungu katika  maisha yote.

“Msikiti huu ukatoe mafunzo yatakayojenga umoja wa watanzania, ukaguse na mioyo yao ya kutekeleza maandiko matakatifu yaliyopo kwenye Quran na yakajenge umoja ndani ya watanzania wote,” alisisitiza.

Aliongeza “ishara hii mliyoionyesha leo ni ya kipekee duniani kote, upendo huu na umoja huu ni wa maajabu sana, tuendelee kushikamana”

Aidha, Rais Magufuli aliwakumbusha watanzania kwenda kupiga kura  Oktoba 28 mwaka  huu kulingana na utashi wa mioyo yao kwa kuchangua viongozi watakaoweka mbele maslahi ya Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charls Mbuge alisema kuwa msikiti huo wenye ofisi ya Mufti umejengwa kwa gharama ya shilingi  milioni 319.28 umekamilika kwa asilimia 100.

“Endapo msikiti huu ungejengwa na mkandarasi basi ungetumia shilingi  milioni 439.43, na umekamilika kwa asilimia 100 na tumeujenga kwa mwezi mmoja na siku 28 tu.”

Aidha, Meja Jenerali Mbuge, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuifanya JKT kuwa karibu na wananchi na kuahidi  kuendelea kutekeleza maagizo pamoja na majukumu  yao kwa ufanisi.

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea msikiti wenye hadhi na sambamba na uamuzi wake wa kurudisha mali za waislamu zilizopotea.

“Umekuwa kiongozi  mwenye kipaji cha kupenda viongozi wa dini na mwenye kumtanguliza Mungu katika Kila jambo. Vitabu vya Mungu  vinasema anayefanyia wema mlipeni na kama hamna cha kumlipa muombeeni.”

Aidha, Mufti Zuberi alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu, huku wakiendelea kuliombea taifa hata baada ya Uchanguzi Mkuu kumalizika.

Itakumbukwa kuwa Agosti 23, 2020, Rais Magufuli aliendesha  harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti  wa Chamwino katika  misa takatifu  ya uzinduzi wa  Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Immaculata   Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, ambapo shilingi millioni 25.6  zilipatikana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments