Majaliwa Apiga Kura Kijijini Kwake Nandagala Wilayani Ruangwa


WAZIRI MKUU na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amepiga kura kijijini kwake Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge mteule wa jimbo la Ruangwa amepiga kura kwenye kituo cha shule ya msingi Nandagala leo asubuhi (Jumatano, Oktoba 28, 2020) akiwa na mkewe Mama Mary Majaliwa.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Waziri Mkuu amesema zoezi la kupiga kura ni haki ya msingi na anamshukuru Mungu kwamba limeenda salama. “Ninamshukru Mungu nimeweza kushiriki haki yangu ya msingi ya kumchagua kiongozi ninayempenda ili aweze kuliongoza Taifa hili.”

“Kwa hapa Nandagala, Mbunge na Diwani walishapita bila kupingwa, kwa hiyo leo nimepiga kura moja tu ya kumchagua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Waziri Mkuu ambaye aliwasili kituoni saa 4:20, na kujipanga foleni yeye na mkewe, alifuata taratibu kama wananchi wengine na akaweza kupiga kura saa 4:53. Aliondoka kituoni hapo saa 5:00 asubuhi.

Akielezea kuhusu utaratibu mzima wa upigaji kura, Mheshimiwa Majaliwa amesema zoezi zima linaendelea vizuri na akawapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa sababu amekuta kuna utulivu na watu wamekaa kwenye foleni wakisubiri kuingia ndani.

Amesema: “Nimekuta watu wanafuata utaratibu, wanapatiwa maelekezo, vitambulisho vinahakikiwa, ni jambo la kujivunia. Amani kwetu bado ni tunu ambayo hatutakiwi kuidondosha chini ikaharibika. Ninatoa wito kwa Watanzania tujitokeze tukapige kura ili tupate viongozi wa ngazi zote ambao watatuongoza. Ni nafasi muhimu, ukiikosa leo, hutaipata tena kwa miaka mitano ijayo,” amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments