CHADEMA WAMBADILISHIA MAJUKUMU TUNDU LISSU… SASA ATAFANYA KAMA MAKAMU MWENYEKITI WA CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema, kitambadilishia majukumu Tundu Lissu, Mgombea wake wa Urais wa Tanzania wakati akiitumikia adhabu ya kutofanya kampeni kwa muda wa siku saba kuanzia jana tarehe 3 hadi 9 Oktoba 2020.

 Akizungumza na waandishi wa habari  leo Jumapili tarehe 4 Oktoba 2020 jijini Dar es Salaam, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema amesema, mbadala wa Lissu kutofanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 katika kipindi hicho, mwanasiasa huyo atapangiwa kazi maalum kama Makamu Mwenyekiti wa Chadema

 “Tundu Lissu siyo tu ni mgombea wa Urais wa chama chetu, huyu ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hivyo hatakosa cha kufanya kwa kipindi cha siku 7.

"Chama kitampangia program mahususi kama Makamu Mwenyekiti kufanya majukumu ya kijamii na kisiasa.”-Amesema

Amesema, Watanzania hawatapata ujumbe wa mgombea wa Urais, lakini wataupata ule wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.

Aidha, Mbowe amesema, Kamati Kuu ya Chadema imeelekeza Kitengo cha Sheria cha chama hicho kuandaa hati ya dharura kwa ajili ya kufungua kesi mahakamani kuipinga adhabu hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments