WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI YA HAYATI BOMANI KWA NIABA YA RAIS DKT. MAGUFULI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mazishi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hayati Mark Bomani kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli na amewataka Watanzania wamuenzi kwa kuuishi utumishi wake uliotukuka wakati wa kupindi chote cha uhai wake.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 14, 2020) wakati alipowaongoza waombolezaji katika kuuaga mwili wa Hayati Bomani kwenye viwanja vya Karimjee na baadaye katika mazishi yaliyofanyika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Serikali imepokea msiba huu kwa huzuni na mshtuko mkubwa.

“Wote sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa Mzee wetu Hayati Mark Bomani alioutoa katika tasnia ya sharia na katika nafasi mbalimbali alizotumikia ndani na nje ya Tanzania. Alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza mzalendo, alisaidiana na Mwanasheria Mkuu wa kipindi hicho Roland Brown katika kutayarisha nyaraka zote za kisheria za Muungano.”

Waziri Mkuu amesemma kati ya mwaka 1965 hadi 1976 aliteuliwa kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza mzalendo nafasi ambayo aliitumikia kwa uaminifu, uadilifu na umahiri mkubwa na alifanikiwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha sekta ya sharia inaimarika.

Amesema Hayati Bomani aliwezesha kupatikana kwa Jaji Mkuu wa Tanzania kutoka nchini Trinidad and Tobago na Mahakimu kutoka Nigeria ili kupunguza uhaba wa watendaji Waafrika katika mhimili wa Mahakama.

Amesema Watanzania watamkumbuka Hayati Bomani kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kamati mbalimbali zilizolenga kupitia sheria na keleta mabadiliko katika sheria. Alikuwa Mjumbe wa Tume ya Rais iliyoundwa kutoa mapendekezo ya mfumo wa demokrasia wa chama kimoja.

Pia, Hayati Bomani alikuwa alikuwa Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Kupitia Sera ya Madini ambayo iliwezesha kutungwa kwa sheria ya madini. Alikuwa mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Kwanza ya Udhamini ya CCM hadi umauti ulipomkuta.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafamilia na waombolezaji wote waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na kila mmoja kwa Imani yake wamuombe Mwenyezi Mungu ampumzishe Hayati Bomani mahala pema.

Hayati Bomani alizaliwa Januari 2, 1932 Bunda mkoani Mara na alikuwa kati ya watoto 10 wa Mzee Bomani na alisoma shule ya msingi Mwamanyili, Nassa ambapo baba yake mzazi ndiye alikuwa mwalimu wake. Alipomaliza shule ya msingi alijiunga na shule ya Wavulana ya Bwiru ambapo alisoma hadi darasa la 10.

Alifaulu na kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya Tabora na ambako pia alifaulu  na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini Uganda mwaka 1953 hadi 1957 ambako alipata shahada ya kwanza ya masuala ya Siasa, Uchumi na Historia. Mwaka 1957 hadi 1958 alijunga na Taasisi ya Ustawi wa Jamii ya The Hague na alitunukiwa diploma ya masuala ya jamii.

Mwaka 1958 hadi 1961 alijiunga na chuo Kikuu cha London nchini Uingereza na kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria. Hayati Bomani mwaka jana aliugua na kupata matibabu nchini Afrika Kusini na India, hali yake ilikuwa nzuri na aliweza kurejea katika kazi alizozipenda za sharia lakini hali yake ilibadilika ghafla na alifariki dunia Septemba 10, 2020 na ameacha mke, Watoto watatu na wajukuu sita.

Mazishi hayo yamehudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mkewe Mama Sitti, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi.


 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527