WAWILI MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA KADA WA CCM NJOMBE




Na Amiri Kilagalila,Njombe
Watu wawili wanashikiliwa na vyombo vya dola mkoani Njombe kwa tuhuma za mauaji ya kada wa Chama cha Mapinduzi na mwenyekiti wa  jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) vyuo na vyuo vikuu mkoa wa Iringa Emmanuel Mlelwa aliyeuawa na kutambuliwa siku 6 baada ya kifo chake.

Akizungumza katika mazishi yaliyofanyika kijiji cha Luvuyo kata ya Madope wilayani Ludewa,mkoani Njombe.Mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya amesema watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo huku wakiendelea na upelelzi wa awali.

Aidha amewata wananchi kuwa wavumilivu kwa sasa kwa kuwa vyombo vya Dola vinaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na mauaji hayo

“Sasa hivi tupo katika kampeni kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu,lakini kampeni haiwezi ikatumika kuvunja amani.Kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,tutawasaka wahusika kwa nguvu zote kuhakikisha wametiwa mbaroni”,alisema Marwa Rubirya mkuu wa mkoa wa Njombe

Vile vile aliema “Maendeleo mnayoayaona katika nchi yetu yanaonekana kwa sababu tuko katika mazingira ya amani,niwaombe wakati serikali tunapoendelea kushughulika na jambo hili niwaombe wananchi tuendelee kuonyesha ukomavu kuhimili jambo hili”, aliongeza Marwa Rubirya

Amewathibitishia wananchi kutoachwa yeyote atakayebainika kuhusika na mauaji hayo “Niwathibitishie kuwa hakuna aliyehusika na uhalifu huu,ambaye hata chukuliwa sheria kwa mujibu wa sheria za nchi yetu”

Nao chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kupitia kwa mwenyekiti wake Jassel Mwamwala kimewataka vijana kuendelea kuwa watulivu kwa kuwa serikali inaendelea kulifanyia kazi swala hilo.

“Na ninyi vijana tunaomba tulieni acheni mihemko serikali yetu inafanya kazi na hakika tutapata jibu”,alisema Mwamwala.

Kijana huyo ameuawa kikatili wiki lililopita na watu wasiojulikana na mwili wake kutambuliwa baada ya siku sita ukiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mji wa Njombe kibena

Marehemu Emmanuel Mlelwa alihudumu kama mwenyekiti wa wanafunzi wa CCM wa vyuo na vyuo vikuu mkoa wa Njombe kabla hajahamia mkoa wa Iringa ambako nako alikuwa akihudumu kwa cheo hicho akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Tumaini kabla mauti hayajamkuta wakati akiwa likizo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527